Home Habari za michezo ‘KITASA CHA KAZI’ CHAKUNJUA NAFSI KWA BENCHIKHA….ISHU NZIMA ILIANZIA ZNZ….

‘KITASA CHA KAZI’ CHAKUNJUA NAFSI KWA BENCHIKHA….ISHU NZIMA ILIANZIA ZNZ….

Habari za Simba leo

Kocha wa Simba SC, Abdelhak Benchikha ameendelea kumpa mzuka beki wa kati wa Simba, Hussein Kazi kutokana na kumuamini na kumchezesha katika mechi nne akitumia kwa dakika 405, huku mwenyewe akisema anaiona safari ya neema ndani ya timu hiyo.

Kazi aliyesajiliwa msimu huu kutoka Geita Gold, hakuwa na nafasi katika kikosi cha kwanza hadi Simba ilipoenda kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 na kocha Benchikha kumpa nafasi akimtumia kwenye mechi tatu na kuonyesha kiwango cha hali juu kilichompa nafasi ya kuanza mechi ya ASFC.

Benchikha alimchezesha kwa dakika 90 katika mechi ya makundi ya Mapinduzi dhidi ya JKU ambapo Simba ilishinda mabao 3-1, kisha akapewa dakika 45 kuivaa Singida Fountain Gate na Simba kushinda tena mabao 2-0 kabla ya kupewa 90 nyingine dhidi ya APR ya Rwanda na mechi kumalizika kwa suluhu.

Baada ya mechi hizo za makundi, Kazi alipewa dakika nyingine 90 katika mechi ya fainali dhidi ya Mlandege na timu hiyo kupoteza kwa bao 1-0, ndipo iliporejea Bara, jana usiku mchezaji huyo alipewa dakika nyingine 90 dhidi ya Tembo FC ya Tabora katika mechi ya hatua ya 64 Bora ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Katika mechi hiyo ya juzi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Benchikha alimtumia Kazi na Kennedy Juma kama mabeki wa kati na timu hiyo kuondoka na ushindi wa mabao 4-0, kitu ambacho kimemfanya beki huyo kuvunja ukimya na kuzungumza kuonyesha furaha aliyonayo na kusema imekuwa ni furaha kubwa kuaminiwa na kocha na kuahidi kutumia nafasi anazopewa kikosini.

Kazi amesema kitendo cha kocha kuendelea kumpa nafasi ya kucheza anamjengea kujiamini na kupata nguvu ya kupambana zaidi, ili huduma yake iifae timu hiyo.

“Si jambo dogo, Simba ina wachezaji wengi, kocha anapokupa nafasi ya kucheza, ina maana anataka ufanye kitu anachoona kinaifaa timu, kadri ninavyocheza naendelea kujiamini na morali inaongezeka,” amesema Kazi na kuongeza;

“Kwenye nafasi yangu kuna wachezaji wenye uzoefu kama Henock Inonga, Che Malone na Kennedy ninapocheza nao, kuna vitu najifunza kutoka kwao.”

Amesema kocha alianza kumpa nafasi kubwa kwenye Kombe la Mapinduzi na tangu hapo alijikuta akibadilisha mtazamo na kujifunza subra ya kuamini ipo siku atakuwa muhimu kikosini.

Hata hivyo, Kazi bado ana kibarua kizito kwani kwa sasa amejikuta akianzishwa kutokana na kukosekana kwa beki Henock Inonga aliyepo katika fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) 2023 na kikosi cha timu ya taifa ya DR Congo, huku beki mwingine Fondoh Che Malone jana alipatwa na dharura muda mchache kabla ya kuanza kwa mchezo huo wa ASFC na nafasi yake kuchukuliwa na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

Kocha Benchikha amekuwa akiwatumia zaidi mabeki hao wa kigeni kwenye nafasi ya beki ya kati, huku Kennedy Juma akiingia na kutoka kwenye mechi za Ligi Kuu na hata ya kimataifa, wakati Kazi huwa anaishia benchi au jukwaani.

Lakini kwa kazi kubwa aliyoionyesha kupitia mechi hizo na kutokuwepo kwa Inonga kikosini, kunamfanya Kazi ataendelea kukaza kila nafasi anayopewa ili kumshawishi kocha kuendelea kumtumia akila sahani moja na mastaa hao.

“Mapinduzi nilicheza dhidi ya JKU kwa dakika 90, Singida Fountain Gate (dakika 45), APR (dakika 90) na Mlandege (dakika 90) na amekuwa akinijenga ili nizidi kupambana zaidi, kama kocha ananipa nafasi basi napambana nisimuangushe,” amesema beki huyo mwenye umri wa miaka 23 na mkataba wa miaka miwili.

Simba ipo Kigoma inatarajiwa kushuka uwanjani leo Jumamosi kuvaana na Mashujaa kabla ya kuhamia mkoani Tabora kucheza na Tabora United siku ya Februari 6 na siku tatu baadaye kurejea nyumbani kula kiporo chao na Azam FC.

SOMA NA HII  TYR AGAIN:- KAMA AL AHLY WALIPATA BAHATI DAR....NA SISI TUNAWEZA KUPATA BAHATI MISRI...