Home Habari za michezo DR CONGO NI KUFA AU KUPONA LEO AFCON…INONGA KUWEKA REKODI HII MPYA...

DR CONGO NI KUFA AU KUPONA LEO AFCON…INONGA KUWEKA REKODI HII MPYA BONGO…

Habari za Michezo

Beki wa Simba, Henock Inonga na chama lake la DR Congo, watakuwa na fursa ya kuondoka kwa heshima nchini Ivory Coast wakati watakapoikabili Bafana Bafana ya Afrika Kusini katika mechi kusaka mshindi wa tatu wa Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 kwenye Uwanja wa Felix Houphouet Boigny leo.

Inonga amecheza kwa kiwango bora katika michuano hii akiwasha katika mechi tano kati ya sita ambazo timu yake imecheza na alikosa mechi moja tu ya hatua ya makundi dhidi ya Taifa Stars ya Tanzania baada ya kuumia katika mechi iliyotangulia dhidi ya Morocco.

Kutokana na ubora aliouonyesha Inonga, anatarajiwa kuanza tena leo katika mchezo huu unaotarajiwa kuwa mkali ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka Afrika baada ya hatua ya nusu fainali ya michuano ya Afcon kumalizika na timu hizo kucheza soka la kuvutia.

Kila timu inataka kuonyesha umwamba wake kwenye hatua hii baada ya zote kutolewa hatua ya nusu fainali ili zisiondoke kwenye michuano hiyo patupu.

Bafana Bafana inayoundwa na wachezaji 10 kutoka katika kikosi cha Mamelodi Sundowns, ilionyesha kiwango kizuri na kuipeleka Nigeria hadi hatua ya penalti, huku DR Congo, yenyewe ikitolewa na wenyeji Ivory Coast kwa kulala bao 1-0 bao pekee la Sebastian Haller wa Borussia Dortmund.

Hii ni mara ya pili DR Congo inacheza mshindi wa tatu kwenye michuano hii kwa miaka ya hivi karibuni baada ya mwaka 2015, kuibuka na ushindi baada ya kuichapa Equatorial Guinea kwa mikwaju ya penalti, hata hivyo, kwa Afrika Kusini ni mara yao ya kwanza wanafanya hivyo tangu mwaka 2000, walipoichapa Tunisia.

Afrika Kusini watamkosa staa wao Grant Kekana ambaye altolewa kwa kadi nyekundu kwenye mchezo dhidi ya Nigeria na nafasi yake inaweza kuchukuliwa na Nkosinathi Sibisi au Siyanda Xulu ambao watacheza pamoja na Mothobi Mvala kwenye eneo la ulinzi wa kati.

Kwa upande wa Congo, ambao wameonyesha kiwango cha juu, Gael Kakuta ambaye alirejea uwanjani kwenye mchezo wa nusu fainali lakini akacheza dakika 45 tu anatarajiwa kuwa mchezaji muhimu kwenye mchezo huu.

Kufungwa: DR Congo wanatakiwa kuwa makini kwani wamesharuhusu mabao matano kwenye michuano ya mwaka huu, huku Afrika Kusini wakifungwa matatu tu.

Kukutana: Timu hizo zimeshakutana mara tano ambapo Afrika Kusini imeshinda michezo mitatu sare moja na Congo imeshinda mmoja.

SOMA NA HII  BAADA YA KUICHAPA MAZEMBE...NABI AWAPA 'MAKAVU' WALIOKUWA WANAMSEMA KUWA NI KOCHA WA LIGI KUU PEKEE...