Home Habari za michezo HIVI NDIVYO BENCHIKHA ANAVYOPITA ‘NYAYO KWA NYAYO’ KWENYE NJIA ZA NABI…

HIVI NDIVYO BENCHIKHA ANAVYOPITA ‘NYAYO KWA NYAYO’ KWENYE NJIA ZA NABI…

Habari za Simba leo

Unamkumbuka kocha aliyerejesha furaha na mataji Yanga, Mtunisia Nasreddine Nabi? Sasa ni kama kocha wa Simba Mualgeria Abdelhak Benchikha anapita njia za Nabi kwenye Ligi Kuu msimu huu.

Akiwa na Yanga, Nabi katika misimu miwili, alibeba makombe yote sita makubwa kwa michuano ya ndani ambayo klabu hiyo iliyakosa kwa muda mrefu kabla ya ujio wake pia aliifikisha katika Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Alibeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili, Kombe la Shirikisho (ASFC) mara mbili na Ngao ya Jamii mara mbili hivyo hakupoteza kitu katika misimu hiyo.

Kocha wa Simba, Benchikha tangu ametua kikosini hapo alipotambulishwa Desemba 2, 2023 amekuwa akipita kwenye baadhi ya njia alizopita Nabi huku kubwa zaidi ikiwa ni namna anavyofanya mabadiliko ya wachezaji (rotation) kikosini kwake.

Mabadiliko ya wachezaji kutokana na aina ya mechi ndiyo ilikuwa siri kubwa ya ushindi kwa Nabi, na sasa Benchikha wa Simba ni kama anapita mule mule.

Hadi sasa Benchikha ameiongoza Simba kwenye mechi sita za Ligi, tatu za Ligi ya Mabingwa Afrika na moja ya Kombe la Shirikisho (ASFC).

Katika mechi hizo ametoa nafasi kwa kila mchezaji (waliopo na walioondoka), kikosini hapo kuonyesha ubora wake. Wote wamecheza.

Kuanzia Desemba 15, mwaka jana zilichezwa mechi chache sana. Ilikuwa ni kipindi cha usajili wa dirisha dogo, michuano ya Kombe la Mapinduzi na fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023, lakini Mchakamchaka ukarejea Januari 31 ambapo Simba ilicheza mechi ya ASFC dhidi ya Tembo FC kutoka Tabora na kushinda 4-0.

Baada ya hapo mikiki mikiki ya Ligi kwa Simba ilirejea kwani Februari 3, iliilaza na Mashujaa 1-0 kule Kigoma Februari 6, ikaichakaza Tabora United 4-0 kule Tabora kisha Februari 9 ikawa mwenyeji wa Azam FC katika sare ya 1-1, pale CCM Kirumba Mwanza na Februari 12 ikaichapa Geita Gold 1-0 kwenye uwanja huo huo.

Katika mechi hizo nne zilizopita Simba imetumia zaidi ya asilimia 90 ya wachezaji wake wote. Mawinga Willy Onana na Ladack Chasimba, Saleh Karabaka waliokuwa na majeraha madogo, makipa Hussein Abel na Ally Salim aliyekuwa mgonjwa, sambamba na Henock Inonga aliyekuwa kwenye Afcon ndio hawajatumika kwenye mechi nne zilizopita.

Mechi zote nne za ligi zilizopita, Benchikha amefanya mabadiliko katika kikosi cha kwanza pia wakati mechi ikiendelea amekuwa akifanya mabadiliko ‘sub’, ambapo kila mechi amefanya ‘sub’ zote, kiufupi wakati mchezo ukiendelea amefanya mabadiliko mara tano kwenye kila mechi.

Mabeki Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Che Malone Fondoh, ndio wachezaji pekee waliocheza dakika zote 360 za mechi nne za Simba zilizopita bila kufanyiwa mabadiliko.

Anayefuata kwa kucheza dakika nyingi katika mechi hizo nne baada ya Tshabalala na Malone ni winga Kibu Denis aliyecheza dakika 346, akifuatiwa na Kiungo Babacar Sarr aliyecheza dakika 300, kisha kiungo mshambuliaji Said Ntibanzokiza akicheza dakika 286 huku Chama akifuatia kwa kucheza dakika 275.

Wengine ni beki Shomari Kapombe aliyecheza dakika 226, kiungo Sadio Kanoute dk 225, beki Kennedy Juma dk 224, na mshambuliaji Pa Omar Jobe aliyekichafua dakika 199 huku mshambuliaji mwezake Freddy Michael akicheza dakika 188. Makipa Aishi Manula na Ayoub Lakred wote wamecheza mechi mbili sawa na dakika 180 kwa kila mmoja, kiungo Fabrice Ngoma amecheza dakika 160 huku mwenzake Mzamiru Yassin amekichafua dakika 147, mabeki Israel Mwenda na Husein Bakari ‘Kazi’ kila mmoja amecheza dakika 135.

Winga Luis Miquissone amecheza dakika 62, wakati beki David Kameta ‘Duchu’ na winga Edwin Balua kila mmoja akicheza dakika 4, na kiungo Abdallah Hamis ndiye mchezaji aliyecheza dakika chache zaidi kwa waliopata nafasi, akikipiga kwa dakika moja pekee katika mechi nne zilizopita za ligi.

Hata hivyo, katika moja ya mahojiano na Mwanaspoti, kocha Benchikha alisema anafanya mabadiliko hayo ili kuwapa nafasi ya kupumzika wachezaji wake lakini pia anataka kila mmoja aonyeshe kipaji chake.

“Tuna mechi nyingi za mashindano tofauti. Lazima tufanye mabadiliko ili kuwapa nafasi ya kupumzika wachezaji.”

SOMA NA HII  RASMI....NABI AFUNGA FAILI LA FEI TOTO YANGA...ATUMA UJUMBE HUU KWA MABOSI JANGWANI...