Home Habari za michezo PAMOJA NA KURUHUSIWA KUTUMIA UWANJA WA MKAPA…SIMBA, YANGA ZAPIGWA ‘MKWARA’…

PAMOJA NA KURUHUSIWA KUTUMIA UWANJA WA MKAPA…SIMBA, YANGA ZAPIGWA ‘MKWARA’…

Uwanja wa Mkapa

Mashabiki wa Soka wameaswa kuheshimu ukarabati unaoendelea Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam watakapokwenda kutazama mechi za kimataifa za Simba SC na Young Africans.

Serikali imeruhusu uwanja huo kutumika kwa mechi za Ligi ya Mabingwa barani Afrika na zile zinazohusisha klabu za Simba SC na Young Africans.

Meneja wa Uwanja huo, Milinde Mahona amesema sehemu ya kuchezea ipo tayari lakini sehemu nyingine zinaendelea na ukarabati lakini kwa vile ni uwanja pekee unaotegemewa kwa michezo ya kimataifa utatumika kwa mechi hizo tu, hivyo mashabiki wanapaswa waheshimu kazi hiyo.

“Watanzania wanapokuja Benjamin Mkapa wahakikishe wanakuja kwa kufuata taratibu zilizowekwa na wajue ukarabati unaendelea hivyo si busara kuanza kuharibu,” amesema Mahona.

Meneja huyo amesema kufanya hivyo watamsaidia mkandarasi kuendelea na kazi na waendelee kutunza vitu vilivyomo uwanjani humo ikiwepo viti ingawa bado havijabadilishwa.

Awali serikali ilitangaza kuufungia uwanja huo sambamba na ule wa Uhuru jambo ambalo lilileta taharuki kwa mashabiki, lakini serikali ililegeza masharti na kuruhusu uwanja huo kutumika kwa mechi za kimataifa pekee.

Jumamosi (Februari 24) Young Africans inatarajiwa kuutumia Uwanja huo kwenye mchezo wa Mzunguuko watano wa Kundi D Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya CR Belouzdad ya Algeria.

SOMA NA HII  AS VITA, TP MAZEMBE WAMLILIA RAIS MAGUFULI