Kocha wa Simba SC, Abdelhak Benchikha, amesema hawataidharau Tanzania Prisons wanaokutana nao leo Jumatano (Machi 06) kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Simba SC leo Jumatano (Machi 06) inakutana na Tanzania Prisons huku ikiwa imetoka kupata ushindi mnono kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika wa mabao 6-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana na kufuzu Robo Fainali ya michuano hiyo.
Benchikha amesema matokeo na sherehe ya Ligi ya Mabingwa Afrika, imemalizika baada ya dakika 90 za mchezo wao na Jwaneng na sasa akili yao ipo kwenye michezo ya Ligi Kuu kwa kuanzia na mechi ya leo Jumatano (Machi 06) dhidi ya Tanzania Prisons.
“Sitarajii kuwa utakuwa mchezo mwepesi, lazima turudi haraka kwenye hali yetu ya kutaka pointi tatu katika michezo yote iliyobaki ya Ligi Kuu, tumefuzu hatua ya Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, lakini hiyo imeisha mara baada ya mchezo.
“Kwa sasa tunataka kuendeleza kasi yetu ya kuwania ubingwa wa Tanzania, ili tufikie huko ni lazima sasa kuhakikisha tunashinda michezo yetu yote,” amesema Benchikha, na kuongeza,
“Hatuwezi kuwadharau Tanzania Prisons kwa kuwa sisi tumetoka kufanya vizuri kwenye mechi ya kimataifa, mpira haupo hivyo, kwenye kila mchezo lolote linaweza kutokea na ndio maana tutakabiliana nao kwa tahadhari huku tukilenga pointi tatu muhimu,” amesema
Amesema wamefanya maandalizi mazuri kuelekea kwenye mchezo huo wa leo Jumatano (Machi 06) na kuwataka wachezaji kusahau matokeo yao na Jwaneng Galaxy na waelekeze akili zao kwenye mchezo wa leo utakaoanza saa 10:00 jioni.
“Ninachoangalia kwa sasa kama kocha ni kuhakikisha kile ambacho tumekuwa nacho, kwa maana ya ubora unaendelea kuwapo kwenye michezo inayofuata tukianza na huu dhidi ya Tanzania Prisons,” amesema Benchikha.
Katika michezo minne baada ya mchezo wa leo Jumatano (Machi 06) dhidi ya Tanzania Prisons, Simba SC itaumana na Coastal Union Machi 9, Singida Fountain Gate Machi 12 na siku tatu baadae wataumana na Mashujaa FC yote ikichezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro isipokuwa dhidi ya Coastal Union ambao utapigwa CCM Mkwakwani jijini Tanga.