Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI NA MEMELOD JUMAMOSI HII…SKUDU ‘KINYOONGEE’ KASEMA HAYA….

KUELEKEA MECHI NA MEMELOD JUMAMOSI HII…SKUDU ‘KINYOONGEE’ KASEMA HAYA….

Habari za Yanga leo

Kikosi cha Yanga kinaendelea kujifua kwa mazoezi makali kikijiandaa na mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, huku nyota wa timu hiyo, Mahlatse Makudubela ‘Skudu’ ambaye ni Msauzi ameamua kuuza siri la wapinzani wao hao.

Skudu aliyewahi kuichezea Mamelodi mwanzoni mwa miaka ya 2010 amewatoa hofu mashabiki wa Yanga kwa kuwaambia kwamba wapinzani wao ni wagumu, lakini ana hakika wanapigika Kwa Mkapa kwani amelisaidia benchi juu ya kukabiliana nao katika mechi hiyo itakayopigwa Machi 30.

Skudu amesema ni kweli Mamelodi ni timu bora, lakini Yanga ina kikosi bora cha kupata matokeo mbele ya Mamelodi na wala hawataingia Kwa Mkapa kinyonge kwani kila kitu juu yao kwa sasa kipo hadharani kwa makocha.

“Nafuatilia taarifa za kwetu na nimeona hata Mamelodi wana hofu na Yanga kutokana na mabadiliko yao makubwa ya hivi karibuni na ubora mkubwa uliopo, huku bahati nzuri tuna uongozi imara, benchi kubwa la ufundi na kikosi kipana na kubwa zaidi ni mashabiki wengi wanaoiunga mkono kwa kila kila mechi, vitu vinavyoitisha Mamelodi kukosa usingizi,” amesema Skudu aliyesajiliwa msimu huu kutoka Marumo Gallants ya Afrika Kusini iliyotolewa nusu fainali na Yanga katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita.

Timu hiyo iliyokuwa Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) kwa sasa imeshuka daraja na Skudu akaibukia Jangwani japo amekuwa hana maajabu kwani amefunga bao moja tu hadi sasa katika Ligi Kuu akiwa na kikosi cha Yanga.

“Naamini kabisa tutashinda uwanja wa nyumbani kwa kishindo na sio kwa kubahatisha tunajulikana uwezo wetu wa kubadilisha mchezo hivyo mashabiki wasihofu tutakwenda kuwashangaza, kwani kila kinachoendelea kule nimekuwa nikishea na wenzangu na tunaifuatilia kwelikweli,” ameongeza.

Yanga inatarajiwa kuvaana na Mamelodi katika mechi itakayopigwa kuanzia saa 3:00 usiku kwenye Uwanja wa Mkapa kabla ya kurudiana Aprili 5, mjini Pretoria na mshindi wa jumla atatinga nusu fainali kucheza na mshindi wa mechi kati ya Esperance ya Tunisia na Asec Mimosay ya Ivory Coast.

SOMA NA HII  SIMBA WAREJEA DAR USIKU WAKITOKEA ARUSHA