BEKI wa Lubumbashi Sport ya DR Congo, Mtanzania Abdallah Shaibu ‘Ninja’ kuna jambo amejifunza kutokana na kupata nafasi ya kucheza nje kwa awamu mbili tofauti, linalompa nguvu ya kutoogopa changamoto anazokutana nazo.
Ninja anasema kwa mara ya kwanza alipoondoka nchini mwaka 2019 kwenda kujiunga na LA Galaxy II ya Marekani kwa mkopo, ilimjengea ujasiri na uthubutu.
“Baada ya kumalizana na Yanga msimu uliopita, timu nyingi za Ligi Kuu Bara zilihitaji huduma yangu, ila nilichagua kupata changamoto mpya nje, ndipo nikasaini Lubumbashi Sport na kuna timu nje na hii ambayo tulikuwa tunataka kwenda kucheza na Abdi Banda ambaye yupo Afrika Kusini ila mambo hayakwenda sawa,” anasema na kuongeza;
“Maisha bila uthubutu ni ngumu kusonga mbele, kwani kabla ya Yanga nilitoka Taifa Jang’ombe ya Zanzibar, kisha nikaonekana na timu ya MFK Vyškov ambayo ikanipeleka kwa mkopo LA Galaxy ya Marekani, nikitoka hapa naweza kwenda kwingine ama nikarejea nyumbani.
“Wakati natoka Marekani, niliwahi kwenda kufanya majaribio kuna timu moja huko Canada, kilichofanya nisifanikishe dili hilo ni baada ya kuingia kwa ugonjwa wa Covid 19, ilinibidi nirejee nyumbani.”
MAISHA YA DR CONGO
Anasema Congo vyakula ni gharama, tofauti na Tanzania akitolea mfano wa nyama kilo moja ni Shilingi 18000, mchele ule wa kupikia vitumbua ambao kwa Tanzania unaweza ukauzwa Sh1,600, Congo zikipimwa kilo tatu ni Sh10,000 hadi Sh12,000.
“Tanzania tumezoea mchele kupimwa kwa kilo, huku sijui wanapimia kitu gani, ukikadiria hicho kipimo ni kama kilo tatu,” anasema na kuongeza;
“Ili ule ushibe tena kwa kujibana siyo kujiachia mara matunda, mboga za majani kwa siku inaweza ikakugharimu 25,000, kila kitu bei ipo juu, nilipata changamoto wakati wa mfungo wa Ramadhani, nilikuwa nafunga peke yangu, hivyo wakati wa kufungulia kupata futari ilikuwa ishu, ila kwa sasa nashukuru Mungu, maisha mengine yanaendelea.
“Kimaendeleo maisha ya Tanzania tumepiga hatua kubwa, mfano huku muda mwingi naona yanatumika majenereta kutokana na kukatika umeme, ni nadra kukaa muda mrefu bila ya umeme kukatika, jambo jingine nililoliona huku ni askari wenye silaha unawakuta kila kona.
“Kuna mgahawa wa Kitanzania, huko wanaonyesha mechi za Ligi Kuu kupitia Azam, mara nyingi tunaenda kuangalia na wachezaji wenzangu, wanapenda jinsi ambavyo wachezaji wanapewa thamani, wanasaka fursa hizo za kuonekana na timu kwa hali na mali,” anasema.
WANAVYOISHI WACHEZAJI
Tanzania imezoeleka wachezaji wengi maarufu kuwa na wafuasi kwenye mtandao wa Instagram. lakini kwa ya DR Congo, ni tofauti, asilimia kubwa wanatumia Facebook, huko ndiko utakutana na watu maarufu mbalimbali.
“Wachezaji ambao nimecheza nao Yanga ambao walitoka Congo, tulikuwa tunawashangaa tukiona wanatumia Facebook, tukaanza kuwafundisha mambo ya Instagram ili kukutana na mashabiki wao,” anasema na kuongeza;
“Congo ndio wameanza kuamka sasa, kuanza kuona fursa zilizopo Insta, kuna wakati mwingine hata mitandao ya klabu zao, hawapo haraka kuweka taarifa zao huko.
“Nilianza kuwaonyesha kwenye mitandao ya Yanga na Simba inavyofanya kazi yake, walikuwa wanatamani kuona timu zao na zenyewe zinawapromoti wachezaji wao, kiufupi kama mchezaji hajatoka nje hawezi kuona thamani ya ligi yetu ilivyo juu.”
Anasema wakati anajiunga na Lubumbashi Sport kwa mara ya kwanza, wachezaji wengi walikuwa wanamshangaa, kutoka Ligi ya Tanzania inayoonyeshwa live na kwenda DR Congo ambako ni mechi chache ndizo zinazopewa uzito.
“Wenzetu kuonyeshwa kwa ligi, wanakichukulia kama fursa kubwa ya kuonekana na mataifa mengine, ukiachana na hilo maisha wanayoishi mastaa wa Yanga na Simba,
wanayatamani hasa wanapoona Wacongo wenzao wanapopata umarufu mkubwa wakija Tanzania,” anasema.