Home Habari za michezo CHAMA NA AZIZ KI WALIVYOMALIZA MICHUANO YA CAF KIBABE…REKODI ZAO NI BALAA…

CHAMA NA AZIZ KI WALIVYOMALIZA MICHUANO YA CAF KIBABE…REKODI ZAO NI BALAA…

Habari za Simba na Yanga

Yanga na Simba zimetolewa katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ila licha ya kutolewa kwao lakini mastaa wa timu hizo Stephane Aziz KI na Clatous Chama wamefanya vizuri kwenye kutengeneza nafasi za kufunga.

Yanga ikiwa jijini Pretoria Afrika Kusini ilitoka tena suluhu katika mchezo huo wa marudiano kisha kupoteza kwa mikwaju ya penalti 3-2, huku kwa Simba ikichapwa 2-0, ugenini na kutupwa nje kwa jumla ya 3-0, baada ya kufungwa 1-0, Benjamin Mkapa.

Kwa mujibu wa mtandao wa Fotmob unaotoa takwimu mbalimbali za soka, Stephane Aziz KI wa Yanga na Clatous Chama wa Simba kila mmoja msimu huu hadi sasa wametengeneza jumla ya nafasi za kufunga mabao 18 wakiwa wamefungana miongoni mwao.

Kiungo wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na raia wa Chile, Marcelo Allende pia ametengeneza nafasi za kufunga 18 sawa na kina Chama, wakiwa wamezidiwa na Mohamed Chibi wa Pyramids ya Misri iliyoaga michuano hiyo mapema aliyetengeneza jumla ya nafasi 19 akiwa ndioye kinara hadi sasa.

Kwa upande wa kutengeneza nafasi kubwa za upatikanaji wa mabao, nyota hao pia wamefungana kila mmoja wao kwa sababu hadi michuano hii inafikia robo fainali wametengeneza tano huku wakimpita, Mohamed Chibi wa Pyramids aliyetengeneza nafasi nne pekee.

Akizungumzia hilo, nyota wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alisema, walichokionyesha wachezaji hao ni kupandisha tu thamani zao.

“Mchezaji mkubwa anaonekana katika mechi kubwa na ukiangalia walichokionyesha ni ishara tosha ya kujitangaza kimataifa, ni jambo ambalo kila mchezaji wenye kiu ya kufikia mafanikio ni lazima ajitoe ili kuongeza thamani yake,” amesema Chambua aliyewika pia na Tukuyu Stars na timu ya taifa, Taifa Stars.

Simba na Yanga zilizocheza robo fainali kwa mara ya kwanza pamoja ndani ya msimu mmoja, zinarudi katika michuano ya ndani ikiziacha Mamelodi na Al Ahly zikienda nusu fainali zikisikilizia kujua itacheza na nani kati ya washindi wa mechi kati ya Petro Atletico na TP Mazembe na ile ya Asec Mimosas dhidi ya Esperance zinazopigwa usiku wa leo.

SOMA NA HII  YANGA YATUA KWA MGHANA, MJADALA MO KUTISHIA KUSEPA SIMBA, NDANI YA CHAMPIONI IJUMAA