Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI vs AL AHLY KESHO KUTWA…HAYA HAPA MAMBO 3 YATAKAYOIBEBA SIMBA…

KUELEKEA MECHI vs AL AHLY KESHO KUTWA…HAYA HAPA MAMBO 3 YATAKAYOIBEBA SIMBA…

Habari za Simba leo

Mchezo dhidi ya Al Ahly juzi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa umeionyesha Simba mambo matatu ambayo kama ikiyafanyia kazi ndani ya muda mfupi uliobaki inaweza kufanya vyema katika mechi ya marudiano na kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Matokeo ya mechi ya juzi ambayo Simba ilipoteza mchezo kwa kufungwa bao 1-0 yanailazimisha kuhakikisha inapata ushindi wa zaidi ya bao moja katika mechi ya marudiano itakayochezwa Cairo, Misri, Aprili 5 ili itinge hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo.

Hata hivyo ushindi huo kwa Simba ugenini utategemea zaidi namna ambavyo benchi la ufundi na wachezaji watarekebisha kasoro tatu ambazo zimejionyesha katika mchezo huo.

Jambo la kwanza ambalo Simba itapaswa kulifanya ni kuongeza utulivu na umakini pindi inapokuwa inashambulia ili iweze kutumia vyema nafasi ambazo itatengeneza kwenye mchezo.

Udhaifu wa Simba katika kutumia nafasi za mabao ambazo imekuwa ikitengeneza kutokana na wachezaji wake kutokuwa makini au kukosa utulivu wanapolikaribia lango la timu pinzani, umekuwa ni tatizo kubwa msimu huu na lilijidhihirisha dhidi ya Al Ahly ambapo licha ya kutengeneza zaidi ya nafasi 10 za mabao ilishindwa kupachika bao lolote.

Kwa nyakati tofauti za mchezo, Saido Ntibazonkiza, Sadio Kanoute, Willy Onana na Pa Omar Jobe walipoteza nafasi nzuri za mabao walizopata ndani ya eneo la hatari na kushindwa kuisaidia timu kushinda.

Ikumbukwe, katika mechi hiyo Al Ahly ilipiga shuti moja lililolenga lango na kufunga, huku Simba ikifanya hivyo mara saba na kutoka patupu. Lakini wenyeji wangeweza kutumia hata kona 11 walizopata kufunga mabao, lakini walishindwa huku wageni wakipata kona moja katika mechi nzima.

Imekuwa ni kama mwendelezo wa Simba kupoteza nafasi inazotengeneza kwani kabla ya hapo, takwimu kwa mujibu wa mtandao wa www.fotmob.com zilionyesha kuwa ni timu iliyokuwa inashika nafasi ya tatu kwa kupoteza nafasi kubwa za mabao kwenye hatua ya makundi ambapo ilifanya hivyo mara 10.

Kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha alikiri kwamba timu yake imemuangusha upande wa ushambuliaji huku akiahidi kufanyia kazi waweze kufanya vizuri katika mechi inayofuata.

“Tunawaomba radhi mashabiki wetu. (Ahly) wamepata nafasi moja wameitumia, sisi tumepata nafasi saba hakuna bao. Tumecheza mechi vizuri. Tulikuwa bora katika maeneo karibu yote, lakini kama hufungi huwezi kupata ushindi. Unapocheza na timu kubwa na ukashindwa kufunga bao ndani ya dakika sita za mwanzo sio jambo zuri,” alisema Benchikha.

“Tutajipanga upya kama kundi na kurekebisha kile tulichokosea na naamini nafasi tunayo maana katika mechi ya marudiano hatutakuwa na cha kupoteza.”

Muundo wa kujilinda pindi inapopoteza mpira ni eneno lingine ambalo Simba inapaswa kulifanyia kazi kabla ya mechi ya marudiano. Katika mechi hiyo Simba ilichelewa kuzuia haraka pale Al Ahly ilipokuwa na mpira na hivyo kuwapa mzigo mzito wachezaji wa safu ya ulinzi na hata bao ambalo lilifungwa na wapinzani wao lilitokana na udhaifu huo.

Hadi wakati Nabil Koka anafunga bao hilo, Al Ahly ilikuwa na wachezaji watano kwenye eneo la hatari huku Simba ikiwa na wanne na hilo lilimpa mwanya mfungaji kujaza mpira kimiani akiwa huru.

Kasi ndogo wakati wa kushambulia ni udhaifu mwingine ambao Simba inapaswa kuufanyia kazi ili kuwanyima fursa wapinzani wao kujipanga na kutibua mashambulizi yao tofauti na ilivyokuwa katika mechi hiyo ambayo Al Ahly walifanikiwa kuwa na namba kubwa ya wachezaji katika eneo lao la hatari hata pale waliposhambuliwa kwa kushtukizwa kutokana na kasi ndogo ya Simba katika ujenzi wa mashambulizi.

Akizungumzia mchezo ujao, nahodha wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ alisema kuwa watajipanga kuhakikisha wanapata matokeo mazuri ugenini.

“Haikuwa siku nzuri kwetu japo tulicheza vizuri na kutengeneza nafasi nyingi ambazo bahati mbaya hatukuweza kuzitumia. Kuna mechi ya marudiano wiki inayofuata ambayo naamini tukijipanga vyema tunaweza kuibuka na ushindi,” alisema.

SOMA NA HII  AL MERRIKH WALIA KUHUJUMIWA, WACHEZAJI NANE WAKUTWA NA CORONA