KLABU YA SIMBA imemuongezea mkataba wa mwaka mmoja beki wake wa kulia, Shomari Kapombe ambao ndani yake una kipengele cha kumuongeza mwaka mmoja mwingine endapo akifanya vizuri.
Hizi ni taarifa za ndani kabisa kutoka Simba hivyo wakati wowote kuanzia sasa klabu hiyo itatangaza kuendelea naye msimu ujao wa 2024-2025.
“Tumemalizana na Kapombe, hivyo bado ni mchezaji halali wa Simba, tutaendelea kufaidi huduma yake na uzoefu wake kwani ni kati ya wachezaji wazawa ambao wana nidhamu ya kutunza vipaji na viwango vyao,” kilisema chanzo kutoka ndani ya Simba.
Kabla ya Kapombe kuongezewa mkataba huo, alikuwa anahusishwa kujiunga na Singida Black Stars na Namungo ambapo mtoa taarifa wetu amebainisha kwamba: “Ni kweli Kapombe alipata ofa mbalimbali za timu za hapa ndani na nje.
“Mashabiki wa Simba waendelee kuamini viongozi wao wanasajili wachezaji wa maana, hivyo msimu ujao utakuwa wa burudani na kufurahia mafanikio.”
Kapombe amekuwa ndani ya Simba tangu Julai 2017 alipojiunga na timu hiyo akitokea Azam FC ambapo amefanikiwa kuipa mataji manne mfululizo ya Ligi Kuu Bara 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021.
Pia amekuwa sehemu ya mafanikio ya timu hiyo kucheza robo fainali tano katika misimu sita ya michuano ya kimataifa tangu 2018-2019 hadi 2023-2024.
Mbavu hii ya Kulia bado itaendelea kuhudumu mitaa ya Msimbazi licha ya kutajwa kuwa umri wake umemtupa mkono, lakini Uongozi wa Simba umeona bado anafaa kuendelea kubakia klabuni hapo.