Home Habari za Yanga Leo JONAS MKUDE MFALME WA MATAJI…MAKOMBE 19, ROBO FAINALI CAF 4, DABI 32…HAKUNA...

JONAS MKUDE MFALME WA MATAJI…MAKOMBE 19, ROBO FAINALI CAF 4, DABI 32…HAKUNA MZAWA ANAYEMKARIBIA

HABARI ZA YANGA-MKUDE

Mwishoni mwa msimu uliopita Yanga ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la FA, huku kiungo wa timu hiyo Jonas Mkude akiendelea kuweka rekodi ya makombe kwenye soka la Tanzania.

Mkude ambaye marafiki zake wanapenda kumuita Nungunungu. Huyu ni kama damu yake ina vinasaba ‘DNA’ vya makombe kutokana na idadi ambayo ameshayatwaa kuanzia ameanza kucheza soka.

Mkude kwa sasa ni mchezaji wa Yanga lakini maisha yake muda mrefu alicheza akiwa na Simba sehemu ambayo alikaa kwa takribani miaka 12 tangu alipopandishwa kutoka timu ya vijana mwaka 2011.

Akiwa Simba alitwaa mataji mengi tu tofauti tofauti lakini pia akiwa na Yanga kwa msimu mmoja tu uliopita, ametwaa makombe mawili akianza na lile la Ligi Kuu Bara kisha Kombe la Shirikisho (FA) alilotwaa Visiwani Zanzibar baada ya Yanga kuifunga Azam kwa mikwaju ya penalti 6-5 linaendelea kuonyesha umwamba.

Ifuatayo ni orodha ya makombe ya Staa huyu Jonas Mkude akiwa Simba, na Yanga kwa vipindi tofauti.

LIGI KUU MARA 6

Mkude ndiye mchezaji anayecheza soka hadi sasa kwenye ligi mwenye mataji mengi zaidi ya ligi akiwa ameyatwaa mara sita.

Mkude alinyayua taji lake la kwanza la ligi msimu wa 2011/12, akiwa na Simba na baada ya hapo alibeba tena mara nne mfululizo kuanzia msimu wa 2017/18 hadi 2020/2021. Hivyo katika mataji 22 ya ligi iliyonayo Simba, Mkude amehusika kwenye matano.

Akiwa na Yanga ametwaa taji la ligi mara moja msimu uliopita na kufikisha jumla ya mataji sita ya ligi katika historia yake.

FA MARA 4

Taji la FA alilonyanyua Mkude mwishoni mwa msimu uliopita akiwa na Yanga limekuwa la nne kwake katika historia.

Awali alitwaa kombe hilo akiwa na Simba kwa misimu mitatu tofauti, 2016/17, 2019,20 na 2020/21.

Msimu wa 2011/2012, 2017/18, 2018/19, 2019/20, 2020/21 Mkude alifika fainali ya Kombe hili akiwa na Simba lakini hakufanikiwa kutwaa kombe.

NGAO YA JAMII 6

Mkude ametwaa mara sita Ngao ya Jamii na mara zote hizo alikuwa na Simba.

Alifanya hivyo mwaka 2011, 2012, 2017, 2018, 2019 na 2020.

Mwaka 2010 na 2021 akiwa na Simba sambamba na mwaka 2023 akiwa na Yanga, Mkude alikosa taji hilo licha ya timu aliyokuwa kufika katika fainali.

MAPINDUZI MARA 3

Staa huyo pia ametwaa Kombe la Mapinduzi mara tatu na mara zote alikuwa na klabu ya Simba.

Kwa mara ya kwanza Mkude alinyanyua taji hilo mwaka 2011 kisha akabeba tena mwaka 2015 na 2022.

Katika miaka ya 2014, 2017, 2019, 2020 na 2021 Mkude akiwa na Simba alifika fainali ya Kombe la Mapinduzi.

KIMATAIFA ROBO FAINALI MARA 4.

Mkude amecheza mechi nyingi za kimataifa kwa ngazi ya klabu lakini hajawahi kutwaa taji ila ni miongoni mwa wachezaji wachache wazawa waliofika mbali katika michuano hiyo.

Mkude anaongoza kwa kufika robo fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wachezaji wazawa akifanya hivyo mara nne.

Mara tatu alikuwa na Simba katika misimu ya 2018/19, 2020/21 na 2022/2023 kisha msimu uliopita akiwa na Yanga.

Pia Mkude amefika robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mara moja msimu wa 2021/22 akiwa na Simba.

MECHI ZA DABI 32

Ukiachana na mataji na mafanikio mengine, pia Mkude anaingia kwenye vitabu vya historia kuwa mchezaji aliyecheza mechi nyingi za watani wa jadi, ‘Dabi’ zinazokutanisha Simba na Yanga.

Mkude amehusika kwenye dabi 32 hadi sasa ambapo 29 alikuwa upande wa Simba na tatu akiwa Yanga.

Moja ya rekodi ya kipekee katika Dabi hizo ni kuhusika katika Dabi zilizomalizika kwa kichapo kikubwa kwa miaka ya hivi karibuni na mara zote alikuwa timu ya ushindi.

Mei 6 2012 Simba iliifunga Yanga 5-0 kwa mabao ya Emmanuel Okwi aliyepachika mawili, Felix Sunzu, Juma Kaseja na Patrick Mafisango na Mkude alikuwa sehemu ya chama la Simba lilioitandika Yanga.

Siku zikasonga, Mkude akahamia Yanga. Novemba 5 mwaka jana Yanga ikalipa kisasi kwa kuichapa Simba mabao 5-1, yaliyofungwa na Maxi Nzengeli mawili, Stephane Aziz Ki, Kennedy Musonda na Pacome Zouzoua. Mkude alikuwa sehemu ya kikosi cha Yanga na kuchekelea.

Kwa mujibu wa Gazeti la Mwanaspoti Mkude alisema mafanikio hayo ameyapata kwa kuwa anafanya kazi yake kwa kujiamini zaidi

“Hakuna siri zaidi ya Mungu, subra, nidhamu, kujituma jitihada binafsi sambamba na kuwa na timu imara,” alisema Mkude mwenye umri wa miaka 31.

Credit: Mwanaspoti/Mwananchi

SOMA NA HII  SMBA, YANGA KUWAJUA WAPINZANI WAO LEO KIMATAIFA.