Home Habari za Yanga Leo PRINCE DUBE APEWA VIATU VYA MAYELE…MWENYEWE AFUNGUKA

PRINCE DUBE APEWA VIATU VYA MAYELE…MWENYEWE AFUNGUKA

Habari za Yanga-Prince Dube

Ni zamu ya Prince Dube ndani ya Yanga. Hivyo ndivyo unaweza kusema baada ya mfupa walioushindwa Kennedy Musonda, Hafiz Konkoni na Joseph Guede katika kuvaa viatu vya Fiston Mayele ambaye alitimka kikosini hapo msimu wa 2022-2023 ulipomalizika akiwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara.

Mayele ambaye kwa sasa anakipiga Pyramids FC ya Misri, amehudumu kwa misimu miwili ndani ya kikosi cha Yanga na kufanikiwa kuwa kinara wa mabao kwenye timu hiyo kwa misimu yote hiyo.

Msimu wake wa kwanza ndani ya ligi (2021/22) alifunga mabao 16 akiwa nyuma kwa bao moja dhidi ya aliyekuwa kinara, George Mpole ambaye alifunga mabao 17 akiitumikia Geita Gold.

2022/23 ndio ulikuwa msimu wake wa pili na wa mwisho ndani ya kikosi cha Yanga kabla kutimkia Pyramids FC, aliondoka akiwa ametupia mabao 17 akifungana na aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Simba, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ wakiibuka wafungaji bora.

Baada ya kuacha rekodi hiyo, Mayele alitimka nchini akiwa ametwaa mataji mawili ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA) sambamba na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2022-2023, kisha akaiacha Yanga ikisafa kusaka mbadala sahihi wa kuziba nafasi yake.

Mayele ndani ya kikosi cha Yanga alicheza kwa kiwango cha juu katika misimu miwili akifunga mabao 33 kwenye Ligi Kuu Bara pekee, nje na michuano mingine ikiwemo ile ya kimataifa ambapo msimu wa 2022-2023 walipocheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, alimaliza na mabao saba akiwa kinara.

Prince Dube

Ndiye mshambuliaji ambaye anatazamwa zaidi kwa sasa kutokana na uzoefu alionao kwenye Ligi ya Tanzania akihudumu kwa misimu minne ndani ya kikosi cha Azam FC.

Msimu wake wa kwanza ilikuwa ni 2020/21 akifunga mabao 14, msimu uliofuata hakuwa bora kwani alikaa sana nje ya uwanja kutokana na kupata jeraha la goti, alitupia bao moja tu.

2022/23 Dube akiwa na Azam FC alifunga mabao 12 na msimu wake wa nne na wa mwisho akicheza nusu msimu alitupia mabao saba kabla ya kuondoka kikosini na kuvunja mkataba na timu hiyo.

Sasa ni mali ya Yanga na anatajwa kuwa anaweza kuwa mshambuliaji tishio ndani ya kikosi hicho kutokana na uzoefu alionao ikiwa ni pamoja na kucheza sambamba na viungo wenye uwezo mkubwa.

Dube atakuwa katikati ya Clatous Chama, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz Ki ambaye ndiye alikuwa kinara wa upachikaji mabao Ligi Kuu Bara msimu uliopita akifunga mabao 21 na kumuacha mzawa Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyefunga mabao 18.

Dube afunguka

Mshambuliaji huyo amesema kazi yake ni kufunga, amesajiliwa na Yanga kwa ajili ya kazi hiyo, hivyo anaamini atakuwa na msimu bora baada ya kupata mapumziko ya muda na sasa anajiandaa kujiweka fiti kwa ushindani.

“Kila mchezaji anatamani kuwa kinara hasa ambaye anacheza eneo la ushambuliaji siwezi kuweka ahadi ya kufunga mabao mangapi, ni mapema sana ila nitafunga sana kwa sababu hiyo ndio kazi yangu,” anasema na kuongeza;

“Kucheza pamoja na Chama, Aziz Ki na Pacome hakuna mchezaji ambaye hatamani kufanya kazi na wachezaji hao wenye uwezo mkubwa, nafurahi kuungana nao kwenye timu moja na naamini tutacheza kwa kushirikiana ili kuweza kuisaidia Yanga ifikie malengo.”

SOMA NA HII  CHADRACK BOKA ANA BALAA HUYO…YANGA ALAMA 3 KIBINDONI