Klabu ya Yanga imefanikiwa kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya TS Galaxy ya Ligi Kuu nchini Afrika Kusini kwenye mechi ya kirafiki ya Mpumalanga Premier Cup iliyopigwa nchini humo.
Bao pekee la mshambuliaji mpya wa Yanga, Prince Dube alilofunga dakika ya 55 akitokea benchi, limetosha kuwapa Wananchi furaha mpaka kipenga cha mwisho cha mchezo huo.
Hili ni bao la kwanza kwa Dube ambaye ni raia wa Zimbabwe tangu ajiunge na Yanga akitokea Azam FC.
Mchezo wa kwanza wa mashindano hayo, Yanga ilichezea kichapo cha bao 2-1 kutoka kwa FC Augsburg ya nchini Ujerumani.
Yanga itashuka tena dimbani Jumapili Julai 28, 2024 kuvaana na Kaizer Chiefs inayonolewa na aliyewahi kuwa kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi ambaye ametua kwenye kikosi hicho msimu huu.