Home Habari za Simba Leo KIPA SIMBA APUNGUZA PRESHA…AWATULIZA MASHABIKI

KIPA SIMBA APUNGUZA PRESHA…AWATULIZA MASHABIKI

Habari za Simba- Abel

SIKU chache baada ya taarifa ya Mlinda Mlango namba moja wa klabu ya Simba, Ayoub Lakred kuripotiwa kuumia na kutarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa angalau wiki sita, kipa mwingine wa klabu hiyo, Hussein Abel, amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kusema kipa yeyote ana uwezo wa kuanza kwenye mchezo.

Abel, aliyesajiliwa na Simba msimu uliopita akitokea KMC, amewapa kongole pia makocha wapya wa timu hiyo akisema wana uwezo mkubwa na hawamfokei mchezaji anapokosea bali wanamuelekeza.

Alisema kwa sasa hakuna kuwa na hofu mchezaji mmoja anapokosekana kwa kuwa kila mchezaji ana uwezo mkubwa wa kuanza kikosi cha kwanza.

“Mashabiki wasiwe na hofu, hata kama mchezaji fulani atakuwa hayupo, bado mchezaji mwingine ana uwezo wa kufanya vizuri akipata nafasi,” alisema Abel na kuongeza,

“Msimu huu nimefurahi wachezaji wengi waliosajiliwa ni vijana kwa hiyo wapinzani wajipange, wachezaji wamekuja na morali nao wanataka umaarufu, wana hamu ya kutwaa makombe, wana njaa ya mafanikio, hivyo watu wajipange kweli,” alitahadharisha kipa huyo ambaye kwa sasa yupo na kikosi cha timu hiyo nchini Misri.

Kuhusu benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Faldu Davids, alisema wana ufundishaji wa aina ya pekee unaopendwa sana na wachezaji wengi kwani ni rahisi kuwaelewa.

“Walimu wetu wanajua kufundisha, wanakupa moyo, unapokosea hawakufokei, wanakuelekeza ili usirudie tana kosa ulilofanya.

Halafu watu wasichokijua kocha wetu ni kocha mchezaji, yeye mwenyewe anaingia ndani anacheza na kuelekeza, hana mambo mengi, tunajivunia kuwa naye na tunaomba Mungu abaki kwa muda mrefu kuendelea kuifundisha Simba,” alisema kipa huyo.

Alisema kwa msimu mmoja aliojiunga na Simba amejifunza vitu vingi ambayo awali alikuwa havifahamu, hivyo kwake ni somo kubwa.

“Nilijisikia faraja kuingia Simba, nilikaa na wachezaji wakubwa wenye uzoefu akina Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein “Tshabalala’, ambao wamenipa ujasiri mkubwa ingawa haukuwa msimu mzuri kwetu, hata hivyo sijacheza mechi za kimataifa lakini ile kuwapo tu kwenye timu ambayo inacheza mechi hizo nimejifunzaa vitu vingi ambavyo nilikuwa sivifahamu kabla. Kusema kweli ukicheza hizi timu kubwa ni shule tosha,” alisema Abel.

Akiizungumzia idara ya makipa, amewahakikisha wanachama na mashabiki kutokuwa na wasiwasi kwani mafunzo wanayoyapata ni ya hali ya juu na ni bora pia.

SOMA NA HII  YANGA YAPORWA KOMBE UWANJANI…JKT QUEENS WABABE