Home Habari za Simba Leo LAKRED HATIANI KUIKOSA DABI YA KARIAKOO…SIMBA NA YANGA

LAKRED HATIANI KUIKOSA DABI YA KARIAKOO…SIMBA NA YANGA

Habari za Simba SC

MLINDA Mlango wa Simba, Ayoub Lakred huenda akakosa mchezo wa Ngao wa Jamii utakaoihusisha timu hiyo dhidi ya Yanga Agosti 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, baada ya kupata majeraha ya misuli ya paja ‘Hamstring’.

Ayoub aliyejiunga na Simba Agosti 11, mwaka jana kwa mkataba wa mwaka mmoja kisha kusaini mwingine Julai 8, mwaka huu, amepata majeraha hayo wakati timu hiyo ikiwa katika maandalizi ya msimu ‘Pre Season’ inayoendelea huko Ismailia Misri.

Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo iliyoweka kambi Misri kwa ajili ya maandalizi ya msimu, zililiambia Mwanaspoti Ayoub huenda akakaa nje ya uwanja kwa muda wa mwezi mmoja hivyo kutia shaka uwezekano wa kucheza mchezo wa ‘Dabi ya Kariakoo’.

“Ni kweli amepata majeraha ya misuli ya paja ‘Hamstring’ ila jopo letu la kitabibu linaendelea kumtibia ili apone kwa haraka, kuhusu muda wa kukaa nje siwezi kusema moja kwa moja ila ni kuanzia wiki nne hadi sita,” kilisema chanzo hicho.

Kwa upande wa Daktari wa Simba, Edwin Kagabo alipotafutwa kuzungumzia jambo hilo ila hakutoa ushirikiano juu ya majeraha ya kipa huyo, huku akiweka wazi taarifa zote zinazoihusu klabu hiyo zinapatikana katika vyanzo vyao vikuu vya habari.

Kwa upande wa Daktari wa Tabora United, Abel Shindika alisema, majeraha ya misuli yanategemea na ukubwa wa jeraha ili kujua mgonjwa atakaa nje kwa muda gani ingawa kiuhalisia sio chini ya wiki tatu hadi nne kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

“Unapopata majeraha ya misuli ya paja huwa unatakiwa kukaa nje kwa muda wa wiki mbili hadi tatu kwa ajili tu ya kupatiwa matibabu, kisha baada ya hapo unaongezewa wiki nyingine mbili za kufanya mazoezi mepesi ya kurudi uwanjani,” alisema.

Ayoub aliyetokea FAR Rabat ya Morocco, ameonyesha kiwango bora kilichomweka benchi aliyekuwa kipa namba moja wa kikosi hicho, Aishi Manula huku makipa wengine wakiwemo, Ally Salim na Hussein Abel wakikosa nafasi ya kucheza mara kwa mara.

SOMA NA HII  SIMBA WAJIBU MAPIGO KUHUSU TUZO ZAO ZA MWEZI