Home Habari za michezo MAJALIWA AING’ATA SIKIO TAIFA STARS AFCON 2017

MAJALIWA AING’ATA SIKIO TAIFA STARS AFCON 2017

Habari za Michezo, Majaliwa

Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa hapendi kuona timu ya taifa ya soka ya Tanzania ‘Taifa Stars‘ ikitolewa mapema katika fainali za Afcon 2027 zitakazofanyika hapa nchini kwa kushirikiana na Uganda na Kenya.

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo wakati akizindua rasmi kamati ya maandalizi ya fainali hizo inayoshirikisha wadau wa sekta tofauti.

“Sisi kama Tanzania tunayo nafasi yetu ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya maandalizi ya awali. Sifa tunayo, uwezo tunao.

“Tunayo timu ya taifa na kwa miaka mingi imekuwa inacheza michezo mingi nje ya nchi na mwenendo wa timu yetu ya taifa inapocheza michezo ya nje mnaujua.

“Uwezekano wa wenyeji kuwa washindi ni mkubwa na inawezekana. Haitopendeza sana sisi kuwa wenyeji halafu baadaye tunageuka kuwa washangiliaji. Lazima tuingie kwenye maandalizi thabiti ya timu ya taifa,” alisema Majaliwa.

Fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2027 zitafanyika katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda ambazo zinaandaa kwa pamoja mashindano hayo.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia alisema kuwa ana imani Taifa Stars itakuwa katika ubora kwenye fainali za Afcon 2027 na itawekwa katika chungu cha pili kwenye upangaji wa makundi ya kuwania kufuzu baada ya mwaka huu kuwekwa katika chungu cha tatu katika upangaji wa makundi ya kuwania kufuzu Agcon 2025.

“Ni matarajio yetu kwamba Afcon itakayofanyika hapa kwamba tutakuwa tunaingia moja kwa moja kama wenyeji lakini tutashiriki katika mechi za kufuzu nina hakika kabisa mwenyezi Mungu atatujalia tunaweza kuwa katika chungu cha pili,” alisema Karia.

Kamati hiyo ya maandalizi ya Afcon 2027, inaongozwa na Leodegar Tenga ambaye ni mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na amewahi pia kuwa Rais wa TFF pamoja na kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya CAF.

Wajumbe wengine ni Ayoub Mohammed Mahmoud (Makamu Mwenyekiti), Neema Msitha (Katibu), Said Kassim Marine (Katibu Msaidizi), Wallace Karia, Suleiman Mahmoud Jabir, Nehemia Msechu, Wilfred Kidao, Ally Mayay, Ameir Mohamed Makame, Naima Said Shaame, Mohamed Abdulaziz, Madundo Mtambo, Jacquline Kawishe, Gilead Teri na Aboubakar Bakhresa.

Wengine ni Profesa Mohamed Janabi, Abubakar Liongo, Thomas Ndonde, Rona Lyimo, Ramadhan Dau, Hassan Mabena, Abdul Nsekela, Jumanne Muliro, Abdul Mhinte, Saleh Ally, Hamad Abdallah, Johnson Pallangyo na Kheri Salum Ally.

SOMA NA HII  TANZANIA KUWA MWENYEJI WA AFCON...WAZIRI ATHIBITISHA...MIUNDOMBINU YA KISASA KUJENGWA