Home Habari za Yanga Leo NABI & GAMONDI KUONESHANA UBABE LEO SAUZI

NABI & GAMONDI KUONESHANA UBABE LEO SAUZI

HABARI ZA YANGA-NABI

KLABU ya Yanga watacheza leo jioni dhidi ya wenyeji wao Kaizer Chief kwenye Uwanja wa Bloemfontein nchini Afrika Kusini, katika mechi ya Kombe la Toyota, mashabiki wengi wa soka wanatarajia mpambano mwingine wa mbinu na ufundi kutoka kwa makocha Miguel Gamondi na Nasreddine Nabi.

Mashabiki wengi Tanzania na Afrika wanataka kuona makocha hao waliojaliwa mbinu za ufundishaji na ufundi nani ataibuka mbabe wa mwenzake.

Vita ya makocha hao inakuja kutokana na Nabi raia wa Tunisia kuwahi kuifundisha Yanga na alipotoka nafasi yake ikachukuliwa na Gamondi raia wa Argentina.

Makocha hao kwa nyakati tofauti wameipa mafanikio klabu hiyo katika kipindi kifupi walichokaa na timu.

Nabi mbali na kuwapa ubingwa wa Ligi Kuu Yanga kwa misimu miwili mfululizo, pia aliifikisha timu hiyo hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika huku Gamondi akifanikiwa kuipa ubingwa wa Ligi kuu msimu uliopita na kuifikisha kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Nabi aliyeifundisha Yanga kuanzia mwaka 2021 hadi 2023, akitokea Al Merrikh ya Sudan, kwa sasa ndiye Kocha Mkuu mpya wa Kaizer Chiefs, akijiunga nayo akitokea FAR Rabat ya Morocco ambayo alitua mara tu baada ya kuondoka Yanga.

Gamondi ndiye aliyechukua mikoba yake Yanga akitokea IR Tanger ya Morocco, na moja kwa moja akaiwezesha Yanga kutinga hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza tangu 1998, na kuipeleka moja kwa moja mpaka robo fainali, ikiweka rekodi ya kufika kwa mara ya kwanza tangu mfumo huo uanzishwe 1997.

Akizungumzia mchezo wa leo, Gamondi alisema haangalii sana matokeo ya ushindi bali kutazama wachezaji wake wanafanya nini uwanjani kwa kile alichowaelekeza pamoja na kujaribu mifumo mbalimbali watakayoitumia msimu huu.

“Tunafuraha kuwa hapa, tupo na wenzetu Kaizer Chiefs kwa ajili ya mechi za kirafiki za kimataifa za ‘Pre season’, kwanza tunawashukuru mashabiki wa timu hii kwa kutupa sapoti na kutushangilia katika mechi yetu ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Mamelodi Sundowns.

Tunakwenda kucheza mechi ya kirafiki, ni mchezo ambao tutautumia kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao, tunaenda kuonyesha burudani, soka safi, tunachezesha wachezaji tofauti tofauti, siangalii sana matokeo, bali timu inachezaje,” alisema Gamondi.

Mara ya mwsiho timu hizo zilikutana mwaka jana, Julai 22, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, katika mechi ya tamasha la ‘Wiki ya Mwananchi’, Yanga ikishinda bao 1-0 lililowekwa wavuni na Kennedy Musonda.

Mechi ya leo itakuwa ya tatu kwa Yanga tangu ifike Afrika Kusini, ambapo ilifungwa mabao 2-1 dhidi ya FC Augsburg ya Ujerumani JUlai 21 kabla ya kushinda kwa bao 1-0 katika mchezo wa pili dhidi ya wenyeji TS Galaxy, Jumatano iliyopita.

SOMA NA HII  KOCHA WA ASEC MIMOSAS AKUBALI KUWAACHIA YANGA KIFAA HIKI...WARABU WANATAMBUA JOTO LAKE...