Home Habari za Yanga Leo YACOUBA ARUDI TENA TANZANIA…AAHIDI MAKUBWA

YACOUBA ARUDI TENA TANZANIA…AAHIDI MAKUBWA

Habari za Yanga

NYOTA wa zamani wa Yanga na Ihefu (sasa Singida Black Stars), Yacouba Songne amerejea Bongo akisaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia Tabora United inayoshiriki Ligi Kuu Bara kwa msimu wa pili sasa.

Yacouba amejiunga na Tabora, akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na AS Arta/Solar7 ya Djibouti aliyojiunga nayo akitokea Ihefu na kufanikiwa kutwaa nayo ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo.

Chanzo cha kuaminika kutoka kwa rafiki wa karibu na mchezaji huyo kimesema kwamba, Yacouba tayari amemalizana na Tabora na siku sio nyingi atajiunga na timu hiyo kujifua tayari kwa msimu mpya wa 2024/25 unaoanza Agosti 16 baada ya kuzinduliwa na michuano ya Ngao ya Jamii inakayopigwa kati ya Agosti 8-11 ikishirikisha watetezi Simba, Yanga, Azam na Coastal Union.

“Yacouba yupo Tanzania ni wiki sasa ana anaendelea na mazoezi ataitumikia Tabora Utd kwa msimu mmoja baada ya kusaini mkataba, ubora na uzoefu wa mshambuliaji huo kwenye ligi ndio sababu kubwa ya kuaminika,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Mbali na Yacouba, Tabora pia imefanya usajili wa maana kwa ajili ya kuhakikisha timu hii haiwezi kurudia makosa ya kucheza mechi za play-off kama msimu uliopita, ina kikosi kizuri na cha ushindi.”

Alipotafutwa Yacouba ili kuzungumza dili hilo alisema ni suala la muda kwa yeye kucheza moja ya timu inayoshiriki Ligi Kuu Bara huku akikataa kuweka wazi ni timu gani.

“Mpira ni mchezo wa wazi sio muhimu sana mimi kutaja timu niliyomalizana nayo, muda ukifika kila mmoja atafahamu kwasababu mpira unachezwa hadharani wataniona ila ni kweli nipo Tanzania na nitacheza Ligi Kuu,” alisema Yacouba.

Nyota huyo kwa mara ya kwanza kucheza Ligi ya Bara ni alipojiunga na Yanga 2020 akitokea Asante Kotoko akaitumikia timu hiyo kwa misimu miwili na baadaye akaibukia Ihefu ambayo aliitumikia kwa miezi sita.

Akiwa na Yanga aliibuka kuwa mfungaji bora wa klabu hiyo msimu wa 2020-2021 kwa kuifungia mabao manane kabla ya kuumia na kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu na alipopona msimu wa 2022-2023 aliibukia Ihefu aliyoifungia mabao matatu.

SOMA NA HII  BAADA YA KUUONA MZIKI WA EL-MERREKH....GAMOND AWASHTUA JAMBO YANGA...