Home Habari za michezo JB, NANDY, BILL NASS WATAMBIA SIMBA NA YANGA LEO

JB, NANDY, BILL NASS WATAMBIA SIMBA NA YANGA LEO

habari za simba na yanga

Kama zilivyo mechi zote za Simba na Yanga, tambo, mbwembwe na majigambo yamekuwa wakiendelea kwa mashabiki wa klabu hizo wakiwamo wasanii mbalimbali wa sanaa ya muziki na uigizaji ambao baadhi yao wametoa utabiri wa mechi hiyo ya 10 kwa timu hizo kukutana katika Ngao ya Jamii tangu mwaka 2001.

Hapa chini ni baadhi ya wasanii hao waliotambiana na kutabiri namna wanavyouona mchezo huo utakavyomalizika Kwa Mkapa, kila mmoja akivutia upande wake…Wasome uone!

JB

Mwigizaji na mtayarishaji mahiri wa filamu nchini, Jacob Stephen maarufu JB amesema haoni sababu ya Simba kuwa wanyonge kwa leo, kwani mechi ni yao kabisa na kwamba Yanga wanakufa tena kama ilivyotokea Mkwakwani Tanga msimu uliopita.

“Siku kama ya leo napendaga kusema tu Simba Bingwa, na tunashinda kwa bao moja tu la kipindi cha pili tu, huyo huyo wanaomtaja taja Debora ndiye atakayewauwa, sisi Simba tumesajili bana we, majirani zetu  wameokota tu,” amesema JB.

MSAGA SUMU

Mtunzi na mwimbaji huyu wa muziki wa Singeli aliye shabiki kindakindaki wa Yanga amesema, haoni wa kuizuia timu hiyo kurejesha Ngao Jangwani baada ya msimu uliopita, marefa kuibeba Simba katika upigwaji wa penalti kwa kipa wa Wekundu, Ally Salim kutoka penalti zote kabla hazijapigwa na Yanga kulala 3-1.

“Leo ni liwalo na liwe kwa Simba lazima wachapike kwa mabao 2-0, Baleke ataingia kipindi cha pili na kutupia moja, huku jingine litawekwa kimiani na Pacome, yaani Yanga hii hatuna wasiwasi tunaingiza timu uwanjani kibabe, tunajiamini na wachezaji wetu wote wako vizuri, na inatakiwa Simba wakae mbali na beki za Yanga wasije pata majeraha maana wako kikazi zaidi,” amesema staa huyo wa Mwanaume Mashine.

INSPEKTA HARUNI

Mkongwe wa muziki wa Bongo Fleva aliyewahi kutamba na Gangwe Mobb aliye shabiki wa Simba, Inspekta Haruni ‘Babu’ amesema kwamba haoni kwa nini Simba isitete Ngao kwa msimu wa pili mfululizo wakati wao ndio wababe wa michuano hiyo hasa kwa usajili iliyofanya msimu huu.

“Hakuna mechi rahisi kama hii ya leo, hivyo kwa Simba kama wachezaji wengi ni wageni hivyo Yanga   wataingia kwa kujiamini, hii mechi leo vijana wanakwenda kupigania heshima ya Simba niamini tunashinda hii game, na uzuri kocha nimeona falsafa yake haiendani na watu wa slowly anataka watu wa chap chap kampa kampa tena watu wanondoka spidi ya kufa mtu, wale wanakufa 2-0,” amesema Babu.

BILLNASS

Nyota huyu wa muziki wa Bongo Fleva anayetamba kwa sasa na Mabosi, ni shabiki wa Yanga na katika tamasha la Wiki ya Mwananchi alikuwa mmoja ya watumbuizaji, bila kupepesa macho amesema;

“Leo wana Yanga tunatembea kifua mbele, tunashinda si chini ya mabao matatu, tena za maana haswaa, Simba tunawafunga na kuwafunga midomo yao na huo usajili wanaosema wamesajili vijana huku sisi Yanga tuna wazee.”

KHALID CHOKORAA

Mwanamuziki huyu nyota wa muziki wa dansi aliye shabiki wa Simba ametamba kwamba haoni kwa nini Mnyama asiondoke na ushindi kwa Mkapa wakati imefanya usajili wa maana na ina wachezaji wenye viopaji vikubwa kulingana na watani wao.

“Nawapa tu siri kwamba wamchunge sana yule Awesu maana namba anayocheza ni attaking midfielder yani namba nane ila anaweza pia kucheza nyuma ya mshambuliaji na maana ya  namba 10 na  kuna muda anaweza kucheza kutokea pembeni kama play macker anaua winga moja kisha anaingia ndani kama alivyokua anacheza chama wakati yupo Simba, ushindi ni lazima kwa Simba, usajili mzuri wachezaji wote wako vizuri.”

NANDY

Mwanadada staa wa muziki wa Bongo Fleva akiwa ni shabiki wa kutupwa wa Yanga amesema anaamini kabisa timu hiyo itashinda Kwa Mkapa kwani ina kikosi bora kilichoongezewa majembe ya maana.

“Nina imani na timu yangu ya Yanga, huwa sisi hatuna hofu tukiwa tunataka kucheza na Simba, hivyo leo Simba lazima ifungwe, siwezi kutabiri mabao mangapi, lakini lazima ujue ushindi upo na ni wa lazima.”

JIMMY MAFUFU

Mwigizaji huyo wa filamu na tamthilia nchini, yeye ni Yanga damu na amesema anaiona kabisa timu hiyo ikitoka na ushindi mnono mbele ya Mnyama anayejitafuta kwa sasa.

“Leo Yanga inaenda kufanya maajabu ya kucheza mpira na sio kufanya utoto, timu iko vizuri na kila mchezaji ana hamu ya kufunga mabao, tuna Aziz KI, huyu anaijulia sana Simba na atatupia mapema sana bao moja huku Pacome akimalizia mengine mawili kuandikisha ushindi wa mabao 3-0,” amesema Mafufu.

MONALISA

Mwigizaji na mtangazaji huyu mahiri, anajulikana na unazi wake kwa Wekundu wa Msimbazi ametamba hana presha na mechi ya leo, licha ya msimu uliopita timu hizo kufungwa nje ndani katika Ligi Kuu pamoja na kwamba ilichukua Ngao pale jijini Tanga na kwamba Yanga ikae kwa kutulia kwani Ubaya Ubwela tu.

“Mie sina maneno mengi acha timu iingie uwanjani ionyeshe wazee mpira unachezwaje, kiukweli usajili huu wa Simba wa sasa hivi una matumani mazuri kwa timu yetu kufanya vizuri msimu ujao na kuhusu kushinda leo wala sio la kuuliza tunashinda leo kwa mabao mengi tu,” amesema Monalisa ambaye jina lake kamili ni Yvonne Cherrie, mtoto wa mwigizaji na mtangazaji mkongwe, Suzan Lewis ‘Natasha’.

Nani atakayecheka au kulia baada ya dakika za pambano hilo litakalochezeshwa na mwamuzi Elly Sasii ambaye mwaka juzi alizihukumu timu hizo katika mchezo mwingine kama huo na Simba kulala kwa mabao 2-1? Tusubiri tuone atakayepatia utabiri wake…!

SOMA NA HII  AWESU AWESU NA MASHAKA BALAA JINGINE SIMBA