Home Habari za Yanga Leo SIMBA NA YANGA KILA MWAKA MATATIZO YALE YALE…KUINGIA UWANJANI CHANGAMOTO…MNAKWAMA WAPI?

SIMBA NA YANGA KILA MWAKA MATATIZO YALE YALE…KUINGIA UWANJANI CHANGAMOTO…MNAKWAMA WAPI?

HABARI ZA MICHEZO, SIMBA NA YANGA

Miaka ya hivi karibuni tunashindana kwa kila kitu. Zama za mitandao ya kijamii, wikiendi hii tulikuwa tunashindana tena katika matamasha mawili ya klabu pacha za Kariakoo Simba na Yanga. Simba Day na Wiki ya Mwananchi. Nani ataujaza uwanja?

Simba na Yanga wote walifanikiwa kuujaza Uwanja wa Benjamin Mkapa ambaye mwenyewe amelala Lupaso. Ukienda katika mitandao ya kijamii unakuta namna ambavyo kila mmoja alikuwa anajitapa kwamba kufika saa sita mchana uwanja ulikuwa umejaa au una zaidi ya nusu ya mashabiki. Haya ni mateso bila ya chuki.

Sidhani kama watu wanawahi kwa ajili ya kwenda kutazama wanamuziki. Nawajua mashabiki wetu. Wanawahi kwa ajili ya kwenda kutazama sehemu mbili kubwa.

Utambulisho wa wachezaji na mechi yenyewe. Utambulisho wa wachezaji upo karibu na kuanza kwa mechi yenyewe. Hiki ndicho ambacho kinawapa mateso makubwa mashabiki.

Kwanini shabiki uingie saa sita mchana katika mechi ambayo inaanza saa kumi jioni au saa mbili usiku? Ni suala la hofu. Suala la kila shabiki kuwa na hofu ya utaratibu mbovu wa namna ya kuingia uwanjani. Kuwa na tiketi hakukuhakikishii kutazama mechi kwenye Uwanja wa Mkapa. Unaweza kuwa na tiketi na ukapigwa virungu usitazame mechi.

Una tiketi mkononi lakini virungu vinakufuata, mbwa wanakufuata, majasho ya watu yanakufuata. Unalazimika kusukumana kwa machozi, jasho na damu ili uweze kuingia uwanjani kuitazama timu yako pendwa. Hadi uweze kuingia jukwaani na kukaa unajikuta umechoka kimwili na kiakili huku ukiwa umechoka.

Haishangazi kuona hata mashabiki wasio na tiketi wanajitokeza Uwanja wa Mkapa kwa sababu wanaamini kwamba suala la kuingia uwanjani ni la mapambano zaidi kuliko kuwa na tiketi mkononi. Kwa wenzetu kama hauna tiketi hauwezi kwenda uwanjani kwa sababu hakuna namna unaweza kuingia uwanjani.

Miaka nenda rudi utaratibu ni mbovu vilevile. Karibu uwanja mzima unaingia uwanjani kwa kupitia mageti yaliyopo upande wa Magharibi. Umeona wapi? Kwa wenzetu maisha ni tofauti. Kila tiketi inampeleka shabiki katika jukwaa analokwenda kukaa. Anaingia katika geti la jukwaa analokwenda kukaa. Kwanini pale Kwa Mkapa yanafunguliwa mageti machache? Ni suala la kutafakari.

SOMA NA HII  TAA ZASIMAMISHA MECHI ZAIDI YA DK 16...TANZANIA VS UGANDA...ISHU NZIMA ILIKUWA HIVI