Home Habari za Yanga Leo YANGA KIBARUANI LEO KUUSAKA UBINGWA WA AFRIKA

YANGA KIBARUANI LEO KUUSAKA UBINGWA WA AFRIKA

habari za yanga-NABI

MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, wanatarajia kukutana na Vital’O kutoka Burundi katika mechi ya kwanza ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa leo kuanzia sa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Vital’0 ndio wenyeji wa mechi hiyo baada ya kukosa uwanja wenye sifa ya kutumika katika michuano hiyo inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) huko nyumbani kwao.

Kuelekea mechi hiyo, Rais wa Yanga, Hersi Said, alisema msimu huu wanataka kuchukua kila kikombe cha mashindano ambayo watashiriki lakini akisisitiza ikiwamo ubingwa wa Afrika.

Hersi alisema Yanga wanahitaji kutwaa taji hilo na wala si kufika hatua ya robo au nusu fainali ya michuano hiyo inayofanyika kila mwaka.

Rais huyo alisema kikosi walichonacho msimu huu kina uwezo wa kubeba kombe hilo kubwa Afrika.

“Kila mashindano ambayo tunashiriki safari hii dhamira yetu ni kubeba kombe, tunaweka mguu katika mechi za Ligi ya Mabingwa, dhamira kubwa na kwa baraka za Mwenyezi Mungu kwa nini tusiwe timu ya kwanza Tanzania kuleta ubingwa wa Afrika?” alisema Hersi.

Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema mechi hiyo haitakuwa rahisi kama ambavyo wengi wanafikiria, lakini amezungumza na wachezaji wake jinsi gani ya kufanya na hasa kutumia vizuri nafasi za kufunga mabao zitakazopatikana ili kuondoka na ushindi.

Gamondi alisema matokeo ya ushindi yatawaweka katika nafasi salama zaidi kuelekea mchezo wa marudiano.

“Tunataka kucheza vizuri na kushinda vizuri pia, ili tusiwe na presha sana katika mechi inayofuata, tunataka mchezo unaofuata uwe rahisi, nadhani hili ndilo kubwa zaidi,” alisema kocha huyo.

Naye Kocha Mkuu wa Vital’0, Sahabo Parris, alisema pamoja na kwamba anaifahamu Yanga kuwa timu nzuri na yenye wachezaji wazoefu, lakini hawaihofii.

Parris alisema amekiona kikosi cha Yanga kilipocheza dhidi ya Simba na Azam hivi karibuni, hivyo amejiandaa vyema kukabiliana nao.

“Mechi huwa hazifanani, msidhani jinsi nilivyojipanga dhidi ya Pamba Jiji katika tamasha la Pamba Day, ndivyo nitakavyojipanga dhidi ya Yanga.

“Nipo hapa kwa wiki nzima, nimeona mechi ya Simba na Azam, zote zikicheza dhidi ya Yanga, nimeona zilikuwa zinakosea wapi, kwa hiyo mimi nimeyafanyia kazi mapungufu ya timu hizo zilipocheza dhidi ya mpinzani wangu, niseme tu tumejipanga kisawasawa kwa mechi hii,” alisema kocha huyo.

Hata hivyo alikiri Yanga ina kikosi kizuri na chenye wachezaji wenye vipaji, lakini hayo yote hayawafanyi waingie woga.

“Tunajua Yanga ni timu nzuri na tunajua msimu uliopita walifika hatua gani, ilikuwa ni robo fainali, lakini haitutii woga kwa sababu nao wana udhaifu wao ambao tumeuona katika michezo yao, tutaitumia kuwaadhibu,” Parris alisema.

Aliongeza wachezaji wake wana morali ya hali ya juu na wako tayari kukutana na wapinzani wao huku akisema kila mmoja ‘anautaka’ mchezo huo.

“Mechi itakuwa ngumu na yenye upinzani mkubwa kutokana na ubora wa timu zote mbili. Lakini kikubwa kinachotakiwa ni utulivu wa kutumia nafasi pale itakapotengenezwa,” alisema kocha huyo raia wa Burundi.

Kocha huyo pia aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Nchini (TFF) kwa kuwakubalia kucheza michezo yao Dar es Salaam.

Nahodha wa Vital’O, Ndayishimiye Hussein, alisema wamefanya maandalizi mazuri na kwa sababu hiyo anaamini watafanya vyema na wanachokisubiri kwa sasa ni muda wa mchezo.

“Malengo yetu ni kupata pointi tatu, tunataka tuwaonyeshe wapinzani wetu wanaweza kufungwa kama zinavyofungwa timu nyingine,” alisema nahodha huyo.

Aliongeza kikosi chake kinaundwa na wachezaji watano kutoka nje ya Burundi wenye uzoefu na mashindano ya kimataifa ambao anaamini watasaidia kupata matokeo chanya.

SOMA NA HII  JOB:- MAMELOD WAMESHAJAA KWENYE MFUMO....5G ITAHUSIKA TU....