Home Habari za michezo RAIS SAMIA AMWAGA MAMILION TAIFA STARS…SIMBA, YANGA NA AZAM WAUNGANA

RAIS SAMIA AMWAGA MAMILION TAIFA STARS…SIMBA, YANGA NA AZAM WAUNGANA

Taifa Stars

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, alisema Rais Samia Suluhu Hassan ataungana na vilabu vya Simba, Yanga na Azam FC kutoa zawadi hiyo maarufu kama ‘Goli la Mama’.

Simba, Yanga na Azam kwa pamoja waliahidi kutoa kiasi cha Tsh Milion tano, kwa kila timu endapo Taifa Stars itashinda mchezo wa kesho dhidi ya Ethiopia kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, mchezo utapigwa majira ya saa 1:00 usiku.

“Rais Samia ataungana na Klabu za Simba, Yanga pamoja na Azam FC kutoa shilingi milioni tano ya ‘Goli la Mama’ kwa kila goli la ushindi litakalofungwa, kwa lengo la kuipa hamasa timu yetu ili ifanye vizuri keshokutwa (kesho),” alisema Msigwa.

Katibu huyo aliwapongeza wasemaji wa klabu hizo kwa ubunifu walioufanya kumuunga mkono Rais Samia kwa kutoa Sh. milioni tano kila moja katika ushindi huo.

Aliwataka wachezaji kupambana na kufuata vema maelekezo wanayoendelea kupewa na benchi lao la ufundi ili wapate pointi tatu, pamoja na kuwaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi uwanjani hapo.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, aliwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi uwanjani kuwapa hamasa wachezaji ili waanze vizuri katika mchezo huo wa nyumbani.

“Timu ya Ethiopia haiwezi kutufunga kutokana na kikosi chetu jinsi kilivyo wachezaji wanapaswa kupunguza presha ili waanze vizuri katika mchezo wetu wa kwanza, naamini kila kitu kinawezekana,” alisema Ally.

Kwa upande wa Meneja wa Habari wa Klabu ya Yanga, Ally Kamwe, aliwaomba Watanzania kununua tiketi kwa wingi ili wakajaze uwanja.

“Msimu huu nimekuja na wazo jipya kwa upande wa hizi klabu tatu kila moja itatoa milioni tano kwa ajili ya kumuunga mkono Rais Samia katika hamasa yake ya Goli la Mama,” alisema Kamwe.

Hata hivyo, Msemaji wa Azam FC, Hashim Ibwe alisema kundi la Stars si gumu, hivyo ina uwezekano mkubwa wa kupata ushindi endapo mashabiki watajaza uwanja,” alisema Ibwe.

Wakati huo huo, Kocha Msaidizi wa Taifa Stars, Juma Mgunda, alisema kikosi hicho sasa kimeiva na kipo tayari kuivaa Ethiopia kesho kwenye mchezo huo wa kwanza wa Kundi H, kusaka tiketi ya kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika.

Akizungumza kwenye mazoezi ya timu hiyo yanayofanyika kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam, Mgunda alisema wachezaji wameimarika kwa asilimia 80, na kilichobaki ni kumalizika asilimia zilizosalia ili wawe fiti asilimia 100.

“Tumeandaa kikosi na wachezaji wako fiti kwa asilimia 80, na tunamalizia siku zilizobaki ili tuwe na asilimia 100 ya kuivaa Ethiopia, tumekuwa tukizungumza na vijana juu ya kuwa na utayari wa kuitetea nchi yao na kuiwakilisha vizuri, wanaonekana wako vizuri na tayari kwa mechi hiyo,” alisema Mgunda.

Akiizungumzia mechi hiyo, alisema lengo walilonalo sasa ni kushinda mchezo huo ili kujiweka kwenye mazingira ya kwenda kucheza tena fainali za AFCON nchini Morocco, kama ilivyokuwa kwa zilizopita nchini Ivory Coast.

“Siku zote jambo lolote ukitaka mwisho wake uwe mzuri ni kufanya mambo mapema, umuhimu wa mechi yetu ni kuanza kushinda na kupata pointi tatu nyumbani ili mbele ya safari tuwe kwenye mazingira rahisi ya kufuzu,” alisema.

Hata hivyo, alisema haitokuwa mechi rahisi kwani hata wapinzani wao watakuja wakiwa na akili kama hiyo, hivyo wao makocha na wachezaji itabidi wafanye kazi ya ziada ili kuhakikisha wanafanya kazi kwa vitendo zaidi.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini ( TFF), Cliford Ndimbo, alisema wametangaza viingilio nafuu ili kila Mtanzania apate nafasi ya kuingia uwanjani kuishangilia Stars ambayo imesheheni wachezaji wenye viwango vya juu.

Haji Salum (Mboto), ambaye alizungumza kwa niaba ya wasanii wa bongo muvi, alisema ni wakati wa kudumisha uzalendo na kuachana na mapenzi ya timu.

Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Frank Ngumbuchi ‘Foby’, alisema kesho ataanza kutoa burudani mapema uwanjani hapo ili wachezaji wapate ari ya kufanya vizuri.

SOMA NA HII  RASMI...SIMBA WAUKATIA TAMAA UBINGWA LIGI KUU...AHMED ALLY 'KINYOONGEEEH' KAFUNGUKA HAYA...