Baada ya kurejea nchini, beki Lameck Lawi amesema hatma ya yeye kuitumikia Coastal Union ipo chini ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya Simba kuendelea kukomaa.
Lawi ambaye alisaini mkataba ndani ya Simba, ameshindwa kuitumikia timu hiyo na badala yake alitimkia Ubelgiji kwa ajili ya kujaribu kwenye klabu ya K.A.A Gent lakini mambo yameenda tofauti, hivyo amerudi Tanzania.
Lawi akizungumzia namna mchakato wake wa usajili ulivyoenda amesema anapitia wakati mgumu sasa kutokana na kukosa nafasi ya kucheza kuendeleza alipoishia msimu uliopita na hatimaye kufikia malengo.
“Siwezi nikawa sawa wakati sichezi na ligi inaendelea, hakuna mchezaji ambaye anapenda kukaa nje ya uwanja wakati anaona ana ,uwezo wa kucheza lakini naamini muda utafika nitacheza,”
Wakati Lawi akifunguka hayo, chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Coastal Union kimeripoti kuwa beki huyo atakuwa miongoni mwa wachezaji watakaocheza mechi ijayo.
“Lawi ni mchezaji wa Coastal Union, ni kweli kamati ilitupa nafasi ya sisi na Simba kumalizana na hilo limefanyika, huyu ni mchezaji wetu na mche-zo ujao mtamuona akiitumikia timu yake aliyoipa mafanikio msimu uliopita,” kimesema chanzo hicho.