Home Habari za Simba Leo UWEZO WA KITASA WA SIMBA…ANATISHA WAPINZANI NI BALAA

UWEZO WA KITASA WA SIMBA…ANATISHA WAPINZANI NI BALAA

HABARI ZA SIMBA-HAMZA

Anaitwa Abdulrazack Mohamed Hamza mwenye uwezo mkubwa sana wa kucheza eneo la kushoto na kulia katika nafasi ya beki wa kati katika ukuta wa mabeki wa Simba chini ya Fadlu Davids.

Hamza ambaye ameanza kuwa kipenzi cha mashabiki wa Simba kutokana na kiwango alichokionyesha akiwa na wekundu hao wa Msimbazi katika michezo ya mwanzoni mwa msimu huku akiibua vita mpya.

Hamza ni ingizo jipya katika dirisha lililopita la usajili, akitokea SuperSport United ya Afrika Kusini hakuwa akipewa nafasi na wengi kabla ya kuanza kuonyesha ubora wake katika mchezo wa mshindi wa tatu kwenye Ngao ya Jamii dhidi ya Coastal Union ya Tanga.

Nyota huyo wa zamani wa Namungo kabla ya kwenda Afrika Kusini, alipata nafasi ya kuvaa uzi wa Simba baada ya Chamou Karaboue ambaye alikuwa akicheza na Che Malone kupata majeraha baada ya mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga ambao walipoteza kwa bao 1-0.

Kocha wa Simba, Fadlu Davids alikuwa na majina mawili katika kikosi chake, Hamza na Hussein Kazi (mabeki wa kati) lakini baada ya programu kadhaa za mazoezi aliamua kuanza na nyota huyo ambaye amezaliwa Machi 23, 2003.

Hamza kushoto huku Che Malone akiwa kulia katika pacha mpya ya mabeki wa kati tofauti kabisa na ile ambayo ilianza kuonekana katika Tamasha la Simba Day.

Utulivu, uwezo wa kunyang’anya mpira na hesabu za kukabiliana na washambuliaji hasa ana kwa ana (1v1) vimemfanya kuanza kuzungumzwa ndani ya michezo mitatu ambayo ameichezea Simba, miwili ikiwa ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ndani ya michezo hiyo, Simba haijaruhusu bao, ilianza kwa kushika nafasi ya tatu kwenye Ngao ya Jamii baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Salehe Karabaka, Hamza na Che Malone walifunga njia za Coastal Union huku pembeni wakicheza Shomary Kapombe/Kelvin Kijili na Mohammed Hussein.

Ubora wake uliendelea kuonekana katika mchezo wa kwanza wa Simba katika ligi wakati wakiibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tabora United kisha akaaminiwa tena dhidi ya Fountain Gate ambapo Mnyama aliendeleza makali yake kwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-0.

Ndani ya dakika 270 alizocheza, Hamza kwa kushirikiana na Che Malone kama mabeki pacha wa kati, Simba haijaruhusu bao.

KINACHOMBEBA SIMBA

Ni nadra kuona beki anayetumia mguu wa kulia zaidi kucheza eneo la beki wa kati kushoto, hilo ndio eneo ambalo lilikuwa likimpa wakati mgumu msimu uliopita Che Malone wakati huo kulia kwake alikuwa akicheza Henock Inonga Baka ambaye kwa sasa anaichezea AS FAR ya Morocco.

Che Malone ni mzuri akicheza beki wa kati lakini kulia hivyo ni kama Fadlu amemtua mzigo nyota huyo wa zamani wa Coton Sport FC ambao alikuwa nao msimu uliopita, amefanya hivyo akiwa na Chamou na hata Hamza.

Achana na urefu wa 5.9ft alionao ambao unamfanya kuwa na uwezo wa kucheza mipira ya juu lakini pia kasi ni kati ya vitu vinavyombeba ukimtofautisha na Chamou ambaye pamoja na uwezo mzuri aliona anaonekana kuwa mzito hivyo hilo linamfanya kufika kwa haraka katika maeneo muhimu wakati wakishambuliwa.

SOMA NA HII  AUGUSTINE OKRAH APEWA THANK YOU YANGA...USAJILI WA MSIMU HUU UNATISHA