Home Habari za michezo MASHINE HII YA KAZI KUTUA SIMBA DIRISHA DOGO…MAMBO NI KIMYA KIMYA AISEE…

MASHINE HII YA KAZI KUTUA SIMBA DIRISHA DOGO…MAMBO NI KIMYA KIMYA AISEE…

Tetesi za Usajili

WAKATI timu yao ikiendelea kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, viongozi wa Simba bado hawajaridhika, kwani wanatajwa kumfuata kiungo mshambuliaji Foday Trawally raia wa Gambia, anayekipiga Klabu ya Cetinkaya TSK ya Uturuki.

Habari zilizopatikana jana kutoka ndani ya klabu hiyo, zinasema mazungumzo baina ya pande mbili yameshaanza na Simba inataka kumpa mkataba wa miaka mitatu mchezaji huyo mwenye miaka 23, ambaye pia ameshazichezea klabu mbalimbali nchini Uturuki, ikiwamo Tuzlaspor FC.

Chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo kinasema kuwa Simba imeamua kuongeza kiungo mshambuliaji anayichezea klabu hiyo iliyopo Ligi Draaja la Pili nchini humo, ili kuwasaidia wachezaji wawili kwenye eneo hilo ambao ni Jean Charles Ahoua na Awesu Awesu.

“Ni usajili unaotokana na matakwa ya kocha, amesema anahitaji dirisha dogo waingie wachezaji watatu wa viwango vya juu vya kimataifa kwa ajili ya mechi kubwa.

“Mchezaji huyu ni kiungo mshambiliaji, ambaye kazi yake itakuwa ni kusimama nyuma ya washambuliaji, kutengeneza nafasi na kutoa pasi za mwisho.

“Skauti yetu imejiridhisha kuwa ni mchezaji bora na anayefaa kwa kazi hiyo, kocha anahitaji kiungo anayetengeneza nafasi rahisi zaidi kwa mastraika na huyu ndiye chagua,” kilisema chanzo hicho.

Mbali na mchezaji huyo, habari zinasema Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, anahitaji pia beki wa kati ambaye ni mrefu na mwenye nguvu kwa ajili ya michezo migumu ya kimataifa kwani anadai mabeki wake tegemeo ni wafupi, hivyo anayekuja anaweza kumsaidia kwa kiasi kikubwa kutengeneza ukuta imara zaidi.

Chanzo kinasema kuwa Fadlu anahitaji pia viongozi kwenda sokoni kusaka straika mmoja ili kusaidiane na Leonel Ateba, huku akipendezwa zaidi uchezaji wa Steve Mukwala uhamie pembeni.

“Kocha anasema anataka Mukwala awe anacheza kama winga kwa sababu ni msumbufu, anakaba, ana mbio na uwezo wa kupiga krosi zenye usahihi na za hatari, kwa hiyo anataka kumhamisha ingawa kuna mechi bado atakuwa akimtukia kama straika wa kati,” alisema mtoa taarifa.

Mara baada ya mchezo kati ya Simba na Yanga uliopigwa Oktoba 19, mwaka huu, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Fadlu alifichua lengo lake la kutaka kukiimarisha kikosi chake kipindi cha dirisha dogo la usajili linalotarajiwa kufunguliwa Desemba mwaka huu hadi Januari, mwakani.

“Si kwamba Yanga ni bora kuliko sisi, bali wana uzoefu tu, tunapaswa kuimarisha kikosi chetu na tunafahamu dirisha dogo lipo jirani, hivyo tutapaswa kuboresha zaidi kikosi chetu kwa kuwa mbio za ubingwa bado zipo wazi,” alisema.

Kabla hata dirisha dogo halijafunguliwa, tayari Simba imeshamaliza na winga, Elie Mpanzu, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ambaye amekuwa akifanya mazoezi na kikosi hicho siku zote kwenye Uwanja wa Mo Arena, Bunju, Dar es Salaam.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alikiri kuwa dirisha dogo kutakuwa na ongezeko la wachezaji wachache, lakini wenye tija na uwezo mkubwa, ila bado muda haujafika wa kulizungumzia hilo, badala yake akili zao kwa sasa zipo kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

SOMA NA HII  GAMONDI AWEKA WAZI SIRI HII YA YANGA