Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI NA WAANGOLA KESHO…KAGOMA ARUDISHA TABASAMU SIMBA…

KUELEKEA MECHI NA WAANGOLA KESHO…KAGOMA ARUDISHA TABASAMU SIMBA…

Habari za simba-Kagoma

HABARI njema kwa wanachama na mashabiki wa Simba ni kwamba, kiungo mkabaji asilia wa timu hiyo, Yusuph Kagoma, amepona na amerejea mazoezini na wenzake kwa ajili ya mchezo wa kesho dhidi ya Bravo do Maquis ya Angola.

Mchezo huo wa raundi ya kwanza, hatua ya makundi, Kombe la Shirikisho, unaotarajiwa kupigwa kesho katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kagoma ameonekana kwenye Uwanja wa Mo Arena Bunju Dar es Salaam, akifanya mazoezi na wachezaji wenzake kuelekea kwenye mchezo huo.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, amekiri jana kuwa mchezaji huyo amepona na yupo fiti kwa ajili ya mchezo huo, kilichobaki ni maamuzi ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids.

“Maandalizi yanakwenda vizuri, mwalimu Fadlu anaendelea kukinoa kikosi chake kuelekea kwenye mchezo wetu na kila kitu kiko sawa sawa, hakuna majeruhi yeyote kwa sasa, wote wameshapona, Abdurazack Hamza aliingia kipindi cha pili katika mchezo wetu uliopita dhidi ya Pamba, Joshua Mutale naye ameshapona, Kagoma tangu kikosi kiliporejea mazoezini amekuwa na wenzake kwa ajili ya kupata utimamu wa mwili na yupo tayari kwa mchezo,” alisema Ahmed.

Kagoma na Hamza, hawakuonekana uwanjani tangu Oktoba 19, mwaka huu, walipopata majeraha kwenye mchezo dhidi ya Yanga uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Hata hivyo, Hamza alionekana akiingia katikati ya kipindi cha pili, Ijumaa iliyopita kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, timu hiyo ilipocheza dhidi ya Pamba Jiji na kushinda bao 1-0.

Mutale aliumia kwenye mazoezi ya kikosi cha Timu ya Taifa ya Zambia, ilipokuwa ikijiandaa na michezo yake ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), na kulazimika kurejea nchini kwa ajili ya matibabu.

Kocha wa Simba, Fadlu amesema kwa sasa yupo kwenye hatua za mwisho za maandalizi ya mchezo huo, ambao alisema utakuwa mgumu, lakini akitaka ushindi wa mabao mengi ili kujiweka vizuri kwenye kundi hilo na kwa michezo inayofauta.

“Ni kundi gumu, tunatakiwa kwanza tuwe na njaa ya kupata ushindi nyumbani, kama tukipata nafasi tuwe tunazitumia kupata mabao mengi ambayo huko mbele yanaweza kutuvusha. Tunawaomba mashabiki wetu waje kwa wingi kutushangilia na kuwasukuma wachezaji ili wapate morali ya kucheza kwa nguvu na kupambana,” alisema kocha huyo raia wa Afrika Kusini akiwa kwenye msimu wa kwanza kuifundisha timu hiyo.

SOMA NA HII  WAKATI YANGA SC WAKIENDELEA KUMNGOJA...FEI TOTO ATIMKIA ZAKE ULAYA...DILI LAKE LIKO HIVI...