Home Habari za michezo KUELEKEA LIGI YA MABINGWA …WAARABU WAANZA KUMTOLEA MACHO AZIZ KI…

KUELEKEA LIGI YA MABINGWA …WAARABU WAANZA KUMTOLEA MACHO AZIZ KI…

Habari za Yanga leo

Nahodha wa Al Hilal ya Sudan, Mohamed Abdelrahman, amesema anategemea mchezo mgumu wakati kikosi hicho kitakapopambana na Yanga Novemba 26 mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi huku akimtaja Stephane Aziz Ki kuwa ni mchezaji hatari.

Al Hilal imepangwa Kundi A ikiwa sambamba na timu za Yanga ya Tanzania, TP Mazembe (DR Congo) iliyochukua taji la mashindano hayo mara tano na MC Alger kutokea Algeria.

Abdelrahman alisema kupangwa kwao na Yanga katika kundi moja ni ishara ya kuonyesha msimu huu utakuwa mgumu kwa pande zote mbili, huku akieleza kikosi hicho cha kocha Miguel Gamondi kimebadilika sana kiuchezaji.

“Itakuwa mechi nzuri na ngumu kwa sababu ni timu ambazo tunajuana, Yanga ya sasa ni tofauti na tuliyokutana nayo mara ya mwisho na kuitoa, tunaiheshimu sana kutokana na aina ya wachezaji na benchi bora la ufundi lililopo,” alisema.

Abdelrahman aliongeza, licha ya faida kubwa waliyonayo ya kuzisoma timu za Tanzania mara kwa mara wanapokuja kuweka kambi nchini, ila haitokuwa rahisi huku akiweka wazi wachezaji wote wa Yanga ni tishio kutokana na ubora walionao.

“Mchezaji ninayeweza kumuelezea kiukweli ni Stephane Aziz Ki, ila wote ni wazuri na tunawaheshimu, kwa sasa akili zetu zipo kwa timu ya taifa ya Sudan kuhakikisha tunafuzu michuano ya CHAN, kisha baada ya hapo tutazungumzia suala hilo.”

Yanga itaanza kampeni zake katika hatua hiyo ya makundi kwa kucheza na Al Hilal Novemba 26 mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku ukiwa ni mchezo wa kisasi kwani mabingwa hao wa Tanzania walitolewa na Wasudani hao msimu wa 2022-2023.

Katika msimu huo wa 2022-2023, timu hizo zilikutana katika hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kusaka tiketi ya kutinga makundi ambapo mechi ya kwanza iliyopigwa Benjamin Mkapa Oktoba 8, 2022 Yanga ilipata sare ya bao 1-1.

Mchezo wa marudiano uliopigwa Oktoba 16, 2022, kwenye Uwanja wa Al-Hilal jijini Omdurman Sudan, Yanga ikachapwa bao 1-0, lililofungwa na nyota huyo na kutolewa kwa jumla ya mabao 2-1 kisha kuangukia Kombe la Shirikisho Afrika na kufika hadi fainali.

Msimu huo ambao Yanga ilifika fainali ilicheza na USM Alger ya Algeria ambapo mechi ya kwanza Dar es Salaam ilipoteza kwa mabao 2-1, Mei 28, 2023, kisha marudiano ikashinda 1-0, Juni 3, 2023 na kukosa ubingwa kwa faida ya bao la ugenini.

Yanga imetinga makundi ya michuano hiyo kwa mara ya pili mfululizo kwa rekodi ya aina yake ikifuzu kwa jumla ya mabao 17-0 katika mechi zake nne za raundi za awali ikiiondosha Vital’O kutoka Burundi kwa jumla ya mabao 10-0 na kuichapa CBE SA ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 7-0.

Kwa upande wa Al Hilal ambayo ilianzia pia hatua za awali kama Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, michezo yake yote imecheza kwenye nchi mbili tofauti ingawa kwa sasa imeweka kambi Mauritania ambako ndiko inashiriki Ligi Kuu.

Al Hilal ambayo inacheza Ligi Kuu ya Mauritania kutokana na changamoto za kiusalama kwao Sudan, hatua ya awali iliiondosha Al Ahly Benghazi ya Libya kwa jumla ya mabao 2-1, kisha raundi ya kwanza ikaitoa San Pedro ya Ivory Coast kwa jumla ya mabao 3-2.

Katika Ligi Kuu Bara Yanga inaongoza kwa pointi 24, baada ya kushinda michezo minane na kuchapwa mmoja huku kwa upande wa Al Hilal iliyocheza mechi tano za Ligi Kuu ya Mauritania, imeshinda nne na kutoka sare moja ikiongoza na pointi zake 13.

Credit:- MwanaSpoti

SOMA NA HII  MWAKINYO: WAZANZIBAR HAWATUTAKI...HUU MUUNGANO UNAUNGANISHA NINI..?