Home Habari za michezo KUHUSU KUTOKUCHEZA…KIBWANA AVUNJA UKIMYA YANGA…’ATUPA DONGO’ KWA GAMONDI…

KUHUSU KUTOKUCHEZA…KIBWANA AVUNJA UKIMYA YANGA…’ATUPA DONGO’ KWA GAMONDI…

HABARI ZA YANGA-KIBWANA SHOMARI

KATIKA misimu ya hivi karibuni, jina la Kibwana Shomary limekuwa likihusishwa na mafanikio makubwa ya klabu ya Yanga, hasa wakati wa utawala wa kocha Nasreddine Nabi ambaye kwa sasa anakinoa kikosi cha Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Kibwana alikuwa mmoja wa wachezaji muhimu wa kikosi hicho kilichoweka historia ya kurejesha furaha kwa mashabiki wa Yanga baada ya miaka minne ya kupoteza ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa watani wao wa jadi, Simba SC.

Akiwa na uwezo wa kucheza katika nafasi mbalimbali za pembeni, Kibwana alileta tofauti kubwa ndani ya kikosi cha Yanga, hata pale alipokuwa akitumika kushoto wakati Djuma Shabani alivyokuwa akicheza kulia.

Alisifiwa kama beki mgumu kupitika na alionyesha hilo katika mechi nyingi ikiwamo mojawapo dhidi ya Simba ambayo alibadilishiwa wachezaji tofauti katika mechi moja lakini aliwatuliza na kupatiwa sifa kuwa “Kibwana anakaba hadi kivuli.”

Hata hivyo, hali ilianza kubadilika kwa Kibwana baada ya msimu wa 2022/23, ambapo Yanga ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Katika kipindi hicho, Kibwana alikuwa sehemu ya kikosi kilichovunja rekodi, akiwa ameshiriki katika zaidi ya mechi 30 za ndani na za kimataifa.

Hata hivyo, ujio wa mchezaji wa Ivory Coast, Kouassi Attohoula Yao, ulibadilisha upepo kwa beki huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar. Kibwana alishindwa kupata nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza licha ya mafanikio yake ya awali.

KAZINI KUNA KAZI
Kibwana alizisoma mapema alama za nyakati. Akatuma ujumbe kwenye mitandao yake ya kijamii mwaka 2023, uliosomeka “Kazini kwangu kuna kazi” mara baada ya usajili wa Yao, akionyesha hali ya wasiwasi na ushindani uliokuwa mbele yake.

Ujumbe huu ulidhihirisha Kibwana alitambua mapema kuwa nafasi yake inaweza kuwa matatani, na ukweli ukadhihirika msimu uliofuata ambapo alikosa kucheza mara kwa mara.
Msimu uliopita ulikuwa mgumu zaidi kwa Kibwana. Alijikuta anasugua benchi, kinyume kabisa cha hali ilivyokuwa awali alipokuwa mmoja wa nguzo za kikosi cha Yanga.

Kwa msimu huu, zipo mechi ambazo hakuwapo hata kwenye orodha ya wachezaji wa akiba, hali iliyoashiria taa nyekundu kwa mchezaji huyo.

Jambo jingine lililomweka Kibwana nje ya kikosi ni maendeleo ya wachezaji wapya waliokuja kushika nafasi yake.

Miguel Gamondi, kocha wa sasa wa Yanga, ameonekana kuanza kumuandaa winga Denis Nkane. Gamondi ameonyesha imani kubwa kwa Nkane, hata akasema wazi kuwa anamuona mchezaji huyo ana uwezo wa kufanya vizuri zaidi katika nafasi ya beki ya kulia.

Aidha, Nkane ameanza kupata muda wa kucheza, hali inayoashiria kuwa Gamondi anaona kama atamkosa Yao basi Nkane awe tayari kucheza nafasi hiyo ambayo amekuwa pia akitumika Dickson Job. Nini kinaendelea kwa Kibwana?

SHIDA IKO HAPA
Wakati Kibwana akicheza, alikuwa bora zaidi kati kujilinda kuliko kushambulia. Hii ni shida kwa soka la kisasa na ndio maana Nickson Kibabage anapata nafasi zaidi ya Kibwana. Kibabage, anapocheza anajua kulinda timu na anapokwenda mbele ni tishio kwa sababu anaweza kufunga na kuasisti pia.

Ubora wa Yao Kouassi katika kushambulia pia tatizo jingine kubwa kwa Kibwana. Yao anaweza kufunga, kuasisti na kutengeneza nafasi kila anapopanda mbele.

Kwa timu kama Yanga ambayo ina nyota wengi wenye ubora wa juu, ni kawaida kucheza kwa kumiliki mpira sana na kushambulia sana, na hili linazifanya timu nyingi kucheza kwa kujilinda zaidi.

Wapinzani kujilinda zaidi kunailazimisha Yanga kuwa na wachezaji wengi wabunifu katika kuzichana ngome na Yao ni mtu sahihi zaidi kwa upande wa kulia. Muulize shabiki yeyote anayehoji kutochezeshwa kwa Kibwana, “ungekuwa Gamondi ungemuacha nje Yao na kumchezesha Kibwana?” Bila ya shaka atakujibu “hapana”. Huo ndio mtihani alionao Gamondi.

CHANGAMOTO NA USHINDANI
Hata hivyo, ni muhimu kutazama hali hii ya Kibwana kwa mtazamo mpana zaidi. Wachezaji wa soka wanapitia vipindi tofauti katika taaluma zao. Kuna wakati wachezaji wanakuwa kileleni mwa ubora wao, na kuna wakati wanapitia changamoto kama hizi.

Kwa Kibwana, inaweza kuwa ni fursa ya kujifunza, kurejea kwa nguvu, au kutafuta njia nyingine za kuonyesha ubora wake.

ITAKUWAJE SASA
Swali ambalo mashabiki wa Yanga wanajiuliza ni, nini kitatokea kwa Kibwana? Je, Gamondi ana mpango wowote naye, au Kibwana anakaribia kuondoka rasmi kwenye kikosi cha Wananchi?

Hili ni jambo linaloleta wasiwasi kwa mashabiki wake ambao walishuhudia jinsi alivyokuwa na mchango mkubwa kwa timu katika misimu ya nyuma.

Kibwana bado ana uwezo wa kurejea katika kiwango chake cha juu endapo atapewa nafasi ya kutosha.

Hata hivyo, mazingira ya sasa yanaonyesha kwamba itakuwa vigumu kwake kupata nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza kwa sababu ya ushindani mkali uliopo. Wachezaji kama Boka kushoto na Yao wamejitokeza kuwa chaguo bora kwa kocha Gamondi, na ni wazi kwamba Kibwana anatakiwa kupambana zaidi ili kurejesha nafasi yake.

Lakini pia, klabu inaweza kumsaidia Kibwana kwa kumpa nafasi ya kujiendeleza zaidi, iwe kwa kumtoa kwa mkopo ili aweze kupata muda wa kucheza katika timu nyingine au kwa kumpa nafasi zaidi kwenye mechi za Kombe la FA.

Hii inaweza kumsaidia kurejea kwenye kiwango chake bora na kuendelea kuwa sehemu ya kikosi cha Yanga.

MSIKIE KIBWANA
Kwa upande wa beki huyo, alisema; “Mimi nipo kambini na naendelea na programu za kocha, kuhusu nafasi mwenye uamuzi wa mwisho ni kocha, muhimu ni kuendelea kupambana nafasi ikipatikana nitaonyesha, siwezi kukata tamaa.”

Credit:- MwanaSpoti

SOMA NA HII  ALIYEMTUNGUA MANULA.....AANZA KUVIMBA KIBABE...ACHIMBA MKWARA WA KUFA MTU...