Katika msimu huu wa ligi kumekuwa na mbinu mpya zinazotumika katika safu ya ulinzi wa klabu ya Yanga, ambapo kocha Miguel Gamondi amemchezesha Denis Nkane kwenye nafasi ya beki wa kulia badala ya nafasi yake ya kawaida kama winga.
Hatua hii imeshangaza mashabiki wengi, kwani Nkane kwa muda mrefu amekuwa akijulikana kwa kasi na ustadi wake wa kushambulia kutokea pembeni.
Uamuzi wa Gamondi unatoa ishara kwamba amemwona Nkane kuwa mchezaji mwenye uwezo wa kuleta faida kiufundi na kimkakati, na anaona hatari ya kumuacha sana nje ya kikosi kwamba ataathiri kipaji kikubwa alichonacho.
Nafasi za ushambuliaji za Yanga zimejaza wachezaji mafundi wa boli, jambo linalompa ugumu Nkane kupenya kikosini na hata Gamondi aliwahi kukiri: “Tuongee uhalisia, tuna wachezaji wengi wa nafasi za ushambuliaji. Nkane ni mchezaji mzuri sana, lakini nafasi za ushambuliaji Yanga zina wachezaji wengi wenye ubora wa juu.”
Kwa kauli hiyo na namna ambavyo, Gamondi anamtumia Nkane, ni wazi kwamba analinda kipaji cha nyota huyo kwa kumtumia kimkakati katika baadhi ya mechi anazotaka kuongeza nguvu kwenye ushambuliaji bila ya kuacha pengo katika safu ya ulinzi.
Katika makala hii, tutachambua mambo yanayomfanya Nkane kuwa chaguo la kipekee na sababu zinazoweza kuwa zimemshawishi Gamondi kumhamishia kwenye nafasi ya ulinzi pamoja na kwamba kwenye kikosi chake yupo beki halisi, Kibwana Shomary ambaye anasota tu benchini.
Gamondi anahitaji kitu tofauti zaidi ndio maana amekuwa akimpa nafasi Nkane hata pale ambapo atakosekana Kouassi Attohoula Yao.
KASI NA KUMUDU MAJUKUMU
Kasi ni moja ya sifa zinazomfanya Nkane kuwa na faida katika nafasi ya beki wa kulia.
Kukiwa na ushindani mkubwa kwenye soka la kisasa, mabeki wa pembeni wanatakiwa kuwa na kasi ili waweze kurudi haraka wanapopoteza mpira, na kwa mchezaji mwenye kasi kama Nkane, Gamondi anapata faida mara mbili beki wa kulia anayesaidia mashambulizi na anayerudi kwa haraka kwenye jukumu la ulinzi.
Kasi ya Nkane pia inamwezesha kumfuata mchezaji wa timu pinzani bila kuchelewa, hivyo kumwezesha Gamondi kupata uimara wa ziada katika safu ya ulinzi.
KUBADILIKA KIUFUNDI
Gamondi anaonekana kuvutiwa na uwezo wa Nkane wa kucheza namba saba, na hivyo kumfanya kuwa na uwezo wa kubadilika kiufundi wakati wa mchezo. Kwa mchezaji ambaye amezoea kucheza nafasi ya winga, Nkane ana mbinu zinazomruhusu kufanya kazi kama beki wa kulia anayeshambulia (wing back).
Kwa upande wa Gamondi, Nkane ana uwezo wa kutoa msaada wa haraka kwenye mashambulizi bila kupoteza uwiano wa safu ya ulinzi, jambo linaloiweka Yanga katika nafasi nzuri ya kudhibiti mpira.
USHIRIKIANO KUPITIA PEMBENI
Kama mchezaji mwenye mbinu nyingi, Nkane anaweza kuchangia kwa kiwango kikubwa kupitia ushirikiano mzuri na wachezaji wa nafasi ya mbele, hasa winga wa upande wake.
Katika mfumo wa Gamondi, Nkane anakuwa kama kiungo wa mpito kati ya ulinzi na ushambuliaji, na anaweza kupanda na kushuka kulingana na kasi ya mchezo kama ilivyokuwa katika mchezo wa ligi dhidi ya Singida Black Stars visiwani Zanzibar.
Uwezo huu wa kucheza na kubadilika kwa nafasi ya ulinzi na ushambuliaji unamwezesha Gamondi kufikia lengo lake la kumiliki mpira na kuweka presha kwa timu pinzani.
KUANZISHA MSHAMBULIZI
Mabeki wa kisasa wanahitaji kuwa na ujuzi wa kutengeneza nafasi za kushambulia, na Nkane amedhihirisha kwamba anaweza kufanya hivyo. Kwenye mfumo wa Gamondi, Nkane anapata uhuru wa kushambulia kutokea pembeni, akipenyeza mipira kwa kupiga pasi za haraka zinazoleta faida kwa washambuliaji wa Yanga.
Mbinu hii ya kiufundi inawezesha timu kuongeza kasi kwenye mipango ya kushambulia, na kufanya mashambulizi ya Yanga kuwa na nguvu zaidi.
UELEWA WA NAFASI
Kuelewa nafasi ni sifa muhimu kwa mchezaji yeyote, na Nkane amedhihirisha kwamba anaweza kufanya hivyo kwa usahihi.
Katika nafasi ya beki wa kulia, anachukua majukumu mapya ya kusawazisha safu ya ulinzi huku akiendelea kusaidia kwenye mashambulizi.
Uelewa wa Nkane kuhusu wakati wa kupanda na kushuka kwenye uwanja unampa kocha Gamondi nafasi ya kujenga timu yenye mfumo wenye uwiano, ambapo kila mchezaji anafanya kazi kwa ushirikiano na kuhakikisha kwamba timu ina nguvu kwa upande wa ulinzi na ushambuliaji.
UAMUZI SAHIHI
Katika nafasi ya beki wa kulia, Nkane amekuwa akionyesha uwezo mzuri wa kufanya uamuzi sahihi, jambo linalosaidia timu kujenga na kuzuia mashambulizi.
Uwezo wake wa kutambua wakati sahihi wa kupanda mbele kwa mashambulizi na wakati wa kubaki nyuma kujilinda unampa Gamondi faida ya kuwa na beki anayeweza kudhibiti kasi ya mchezo.
Hii ni muhimu, hasa katika ligi yenye ushindani mkubwa, ambapo timu zinahitaji wachezaji wenye umakini na weledi wa hali ya juu.
MSIMAMO WA GAMONDI
Katika mahojiano na vyombo vya habari, Gamondi alieleza kuwa anapendelea mabeki wa pembeni ambao wanaweza kushambulia na kurudi haraka.
Alieleza kwamba mfumo wake unahitaji mabeki wanaoendana na kasi ya soka la kisasa, na Nkane ameonyesha kuwa ana sifa hizo.
“Tunataka timu yetu iwe na uwezo wa kushambulia kwa kasi lakini pia kurudi haraka kuimarisha ulinzi wetu,” anasema Gamondi, akionyesha wazi kuwa mabadiliko haya ameyapanga kimkakati.