HUKU Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, akisema hatafanya mazoezi yoyote ya mbinu wakiwa Algeria ili kutowapa nafasi wapinzani wao, CS Constantine kufahamu mfumo watakoutumia, kipa, Aishi Manula, ameugua ghafla na kulazimika kubakia Tanzania.
Manula alikuwa ni sehemu ya wachezaji waliotakiwa kuelekea Algeria kwa ajili ya kuwavaa wenyeji CS Constantine katika mechi ya Kundi A ya mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayochezwa Jumapili nchini humo.
Fadlu alisema kuwabadala yake atakuwa na kazi ya kusimamia mazoezi ya kuwaweka fiti kimwili wachezaji wake kwa kuchezea mpira tu.
Kocha huyo alisema maandalizi yote muhimu ya mchezo huo yalimalizikia wakiwa Tanzania, kinachofanyika ugenini ni kuondoa uchovu wa safari.
“Tutakachokifanya ni kuhakikisha wanakuwa sawa upande wa utimamu wa mwili tu, kwa sababu ni hatari kufanya mazoezi ya mbinu ya mchezo huo kwa sasa. Tulimaliza mazoezi ya kimbinu pamoja na kuyafanyia kazi mapungufu na ubora wa wapinzani wetu tukiwa Tanzania.
Huku yatakuwa ni mazoezi ya kawaida tu ya kuweka miili sawa kwa sababu macho yatakuwa mengi kututazama, siwezi kufanya mazoezi ya kimbinu au chochote kile kinatachowafanya wapinzani wetu hata kuhisi tunacheza vipi,” alisema kocha huyo.
Aliongeza moja kati ya maandalizi waliyoyafanya pamoja na kufanyia kazi wapinzani wao ni kuimarisha safu ya ulinzi pamoja na kiungo wa ulinzi kwa kuzingatia watakuwa ugenini.
“Tunatakiwa tuwe vizuri zaidi katika eneo la kuzuia huku tukijiepusha kufanya makosa mengi. Tumefanya mazoezi ya kuimarisha safu ya ulinzi na nafasi ya kiungo wa kukaba kwa sababu tunacheza ugenini, pia tunatakiwa kushambulia kwa haraka tukiwa na mpira na kurudi mapema,” Fadlu, kocha huyo raia wa Afrika Kusini alisema.
Alisema kwa ushirikiano wa pamoja kati ya mabeki, viungo na washambuliaji, kama wakifanya majukumu ya kulinda na kushambulia kwa pamoja, anaamini wataibuka na ushindi katika mchezo huo muhimu.
“Najua mechi itakuwa ngumu kwa sababu Algeria ni moja kati ya nchi zenye ligi bora Afrika, huku bingwa wake mara nyingi huwa hatabiriki, timu yoyote ile inaweza kuwa bingwa tofauti na nchi nyingine ambazo baadhi ya timu zimejitwalia ufalme,” aliongeza Fadlu.
Nahodha wa Simba, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’, alisema wamekwenda kupambana na ajili ya timu yao pamoja na nchi kwa ujumla.
“Tunakwenda kupambana kwa ajili ya Simba na Tanzania, ni mechi muhimu na ngumu sana, kila timu ilipata ushindi katika mchezo wa kwanza. Wachezaji tunafahamu ugumu wa mchezo, ila hatuwaogopi kwa sababu wako kwao kwa sababu Simba ni wazoefu kucheza na timu za Afrika Kaskazini. Hatuna wasiwasi hata kama watakuwa kwao mbele ya mashabiki wao, kupata ushindi ugenini inawezekana, tumeshawahi kushinda nje ya uwanja wetu wa nyumbani,” alisema beki huyo wa kushoto wa Simba na Timu ya Taifa (Taifa Stars).
Wakati huo huo, Manula ameshindwa kuendelea na safari baada ya kupata matatizo ya kiafya dakika chache kabla ya kuanza safari ya kuelekea Algeria.
Maneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema Manula ameshindwa kuendelea na safari hiyo kutokana na sababu hizo, hivyo kikosi kiliondoka na wachezaji 21 badala ya 22 ambapo sasa makipa waliosafiri ni Moussa Camara na Ally Salim.