Home Habari za michezo SAA CHACHE BAADA YA KUTUA ALGERIA….HII HAPA KAULI YA YANGA KUHUSU HALI...

SAA CHACHE BAADA YA KUTUA ALGERIA….HII HAPA KAULI YA YANGA KUHUSU HALI YA MECHI…

HABARI ZA YANGA

WAKATI kikosi cha Yanga kikitua salama nchini Algeria, uongozi wa timu hiyo umesema wako kamili na hawana wasiwasi wowote kuelekea mechi ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji MC Alger utakaochezwa keshokutwa mjini Algiers.

Yanga itashuka katika mechi hiyo ya pili ya hatua ya makundi ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 2-0 na Al Hilal ya Sudan, mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam wiki iliyopita.

Msemaji wa Yanga, Ali Kamwe, alisema kikosi chao kimesafiri vyema na kila mchezaji yuko katika hali nzuri kwa ajili ya kuipambania timu yao.

Kamwe alisema wanatarajia kukamilisha programu ya mazoezi kuelekea mechi hiyo itakayokuwa chini ya benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Mkuu, Sead Ramovic.

“Sisi uzuri tunakwenda Algeria mjini, tukifika pale benchi letu la ufundi litaangalia tunaanzia wapi, tunasiku chache zimebaki kabla ya mechi yetu, ” alisema Kamwe.

Aliongeza wanafurahi kuona mechi yao itachezwa kwenye Uwanja wa Julai 5, 1962 baada ya maombi ya kuhamishiwa kwenye Uwanja wa Ali la Pointe kukataliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Inaelezwa MC Algers iliamini kuupeleka mchezo huo ulioko katika Mji wa Douera uliopo kilomita 19 kutoka jijini Algers wangekuwa kwenye mazingira bora zaidi ya kupata ushindi.

Taarifa kutoka CAF zinasema mchezo huo utachezwa kwenye uwanja uliopangwa na kupitishwa na CAF awali.

CAF imewafungia MC Algers kucheza michezo minne bila mashabiki kutokana na makosa ya utovu wa nidhamu yaliyoonyeshwa na mashabiki wao katika mechi ya mwisho ya kufuzu hatua hiyo ya makundi waliyocheza dhidi ya US Monastir ya Tunisia.

Wakati huo huo kiongozi aliyetangulia Algeria aliliambia gazeti hili maandalizi ya kupokea msafara wa timu yao yamekamilika na wanatarajia kila kitu kitakwenda vizuri.

Chanzo hicho kilisema kwa sasa Yanga haina hofu ya kucheza ugenini kutokana na uzoefu waliokuwa nao katika kukabiliana na changamoto za aina yoyote.

“Tunatarajia kuipokea timu mchana huu (jana mchana) na mchezo utachezwa kama ilivyopangwa awali kwenye uwanja wa Julai 5, tumejiandaa kuwapa furaha mashabiki wetu,” alisema kiongozi huyo.

Chanzo hicho kiliongeza Yanga inatarajia kushuka uwanjani kuwakabili Waarabu hao kwa utulivu na tahadhari, kwa sababu wanajua kila timu inahitaji pointi tatu za kujiimarisha kwenye kundi lao.

Aliongeza wachezaji wote walioko katika mpango kuelekea mechi hiyo wamesafiri na wanaamini watapambana kusaka matokeo chanya.

Kabla ya kuanza safari hapa nchini, Ramovic aliweka wazi amekiandaa kikosi chake kucheza kwa tahadhari kwa sababu malengo yao ni kufanya vizuri katika mechi hiyo ya Kundi A.

Yanga wamepania kupata ushindi katika mchezo huo ili kufufua matumaini ya kucheza hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara wanaburuza mkia katika msimamo wa kundi lao linaloongozwa na Al Hilal inayofundishwa na Mkongomani Florent Ibenge.

SOMA NA HII  KISA YANGA KUKUTANA NA WASAUZI...ABDI BANDA AIBUKA NA HILI JIPYA...'AMFUNDISHA KAZI' NABI...