Home Habari za michezo BAADA YA KUPOTEANA JUZI…..KOCHA YANGA AFUNGUKA WACHEZAJI WALIOMKWAMISHA…

BAADA YA KUPOTEANA JUZI…..KOCHA YANGA AFUNGUKA WACHEZAJI WALIOMKWAMISHA…

Habari za Yanga SC

Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, amesema makosa mawili ya wazi waliyoyafanya dhidi ya MC Alger, ndiyo yaliyowagharimu zaidi na kusababisha kupoteza mchezo, juzi.

Yanga ikiwa Algeria katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika Kundi A uliochezwa Uwanja wa 5 July 1962, ilipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya MC Alger kikiwa ni kichapo cha pili baada ya awali nyumbani ku-pata matokeo kama hayo mbele ya Al Hilal.

Akizungumzia mchezo huo, Ramovic raia wa Ujerumani ambaye hiyo ilikuwa ni mechi yake ya tatu tan-gu akabidhiwe kikosi hicho Novemba 15 mwaka huu, alisema hayakuwa matokeo ambayo waliyatarajia hasa baada ya kuruhusu mabao ambayo yalitokana na makosa yao kwa kupoteza umakini kwenye matukio mawili tofauti.

“Inawezekana haikuwa siku nzuri kwetu, ukitazama tulivyoanza mchezo na matokeo tuliyoyapata ni vitu viwili tofauti, tulifanya makosa mawili ya kupoteza umakini na yakatugharimu, hizi ni mechi ambazo unatakiwa kucheza ukiwa timamu kwa muda wote wa mchezo,” alisema Ramovic.

Wakati Ramovic akiyasema hayo, kuna mambo yameonekana kuchangia zaidi Yanga kupoteza mchezo huo huku wakiwa na hesabu mpya katika mechi nne zilizosalia.

Baada ya kucheza dhidi ya Al Hilal nyumbani kisha MC Alger ugenini, Desemba 14 mwaka huu Yanga itakuwa ugenini nchini DR Congo kukabiliana na TP Mazembe.

Mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa TP Mazembe uliopo Lubumbashi, Yanga inapaswa kuamkia hapo kwani hivi sasa inaburuza mkia ikiwa haina pointi.

Hata hivyo, haitakuwa rahisi kwa Yanga kwenda DR Congo na kushinda, lazima wafanye kazi ya ziada.

Mchezo huo unatukumbusha mwaka 2016 na msimu wa 2022-2023 ambapo timu hizo zilikutana katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi.

Katika mchezo uliopigwa Lubumbashi mwaka 2016, wenyeji TP Mazembe walishinda 3-1 na hata wali-pokuja Dar wakashinda tena 1-0.

Msimu wa 2022-2023, ilikuwa zamu ya Yanga kulipa kisasi kwani nayo ilipata matokeo kama hayo. Mechi ya kwanza ugenini ilishinda 1-0, nyumbani ikashinda 3-1 ikiwa pia ni hatua ya makundi.

Wakati TP Mazembe ikiifunga Yanga nje ndani mwaka 2016 na kuongoza kundi kwa kukusanya pointi 13 huku Yanga ikimaliza mkiani na pointi nne, pia Yanga nayo msimu wa 2022-2023 iliongoza kundi kwa pointi 13, TP Mazembe ikiburuza mkia na pointi tatu.

Pasi zimepotea

Angalia pasi ambazo zilikuwa zinapigwa na viungo wa Yanga ambao walikuwa wakianzisha mashambu-lizi, Duke Abuya, Maxi Nzengeli, Stephanie Aziz KI na hata Mudathir Yahya kwa wakati fulani.

Yanga ilipoteza pasi nyingi ambazo ziliwapunguzia ubora wa kukamilisha mashambulizi yao ya haraka, kwa soka la mashambulizi ya kushtukiza ili ufanikiwe unatakiwa kuhakikisha pasi zako zinakuwa za uhakika kuhakikisha mashambulizi yako yanafanikiwa kitu ambacho Yanga walikikosa.

Kushoto kunavuja

Yanga itaendelea kukumbuka uwepo wa beki wake wa kushoto Chadrack Boka ambaye anapambana kurudi akitokea kuuguza majeraha na hili linakuwa rahisi kutokana na mbadala wake Nickson Kibabage kushindwa kufanya kazi kwa uhakika.

Kibabage ameshindwa kuonyesha akili yake imekomaa baada ya kucheza vibaya mechi mbili mfululizo za mashindano hayo makubwa ya klabu Afrika.

MC Alger walitumia eneo hilo kupitisha mashambulizi yao mengi na kufanikiwa kutengeneza ushindi wao wa kwanza katika mechi mbili ilizocheza.

Ni wazi kwamba Boka ni mtu muhimu katika eneo la ulinzi wa kushoto ukizingatia kwamba anaweza kupandisha mashambulizi huku silaha yake kubwa ikiwa ni kasi na kuzuia yupo vizuri.

Aziz KI amepotea

Kila timu ina injini yake ya kutengeneza mashambulizi, ukiangalia msimu uliopita Yanga ilikuwa inategemea ubunifu mkubwa wa Aziz KI kufanya mambo makubwa lakini msimu huu kiungo huyo ameendelea kucheza kwa kiwango cha chini.

Aziz KI ameshuka na hata uso wake unaonyesha kuwa ni mchezaji anayehitaji muda kurudisha kiwango chake cha msimu uliopita. Kuna mambo mawili yanaweza kufanyika, Clatous Chama achukue majuku-mu ya Aziz KI kwa kuanza kikosi cha kwanza au kiungo huyo kupumzishwa kabisa mechi kadhaa ili ku-rudisha ubora wake kwani anaonekana amechoka baada ya msimu uliopita kutumia nguvu nyingi katika kuwania Tuzo ya Ufungaji Bora wa Ligi Kuu Bara na kufanikiwa kwa kufunga mabao 21.

Majeraha

Yanga bado inateswa na majeruhi walionao kwenye kikosi ambao wameondoa ubora wa timu hiyo ku-cheza kwa kiwango kikubwa, mechi hizi mbili imewakosa Khalid Aucho, Dickson Job na Boka, huku kipa Djigui Diarra akicheza mchezo wa juzi akiwa na majeraha, hii itaiathiri Yanga katika mechi inazoendelea kuzicheza. Hapa hakuna tiba ya moja kwa moja, ishu ya majeraha huwa inaisumbua timu yoyote, kikubwa wachezaji wanaochaguliwa kuziba mapengo ya wanaokosekana wanapaswa kuwa tayari mu-da wote.

Umaliziaji

Kule mbele nako Yanga bado haina utulivu mkubwa wa kumalizia nafasi inazotengeneza, juzi ilianza na mshambuliaji Kennedy Musonda licha ya kuongeza kitu lakini bado kushuka kwake chini sana kuliifanya timu hiyo kuwapa utulivu mkubwa mabeki wa timu pinzani.

Prince Dube anaonekana kupoteza kujiamini, Clement Mzize amekosekana kwa sababu ya majeraha wakati Jean Baleke hana nafasi kubwa. Hao ndio washambuliaji wanaotakiwa kulichukua jukumu hili moja kwa moja na si mtu mwingine.

SOMA NA HII  SENZO AFUNGUKA MAPYA KUHUSU USAJILI WA MORRISON YANGA NA KUONDOKOKA KWAKE..."UONGO HUPEWA SANA NAFASI TZ"...