Home Habari za michezo KUHUSU KIWANGO CHA MPANZU…FADLU AFUNGUKA A-Z…AITAJA YANGA🤭🫣…

KUHUSU KIWANGO CHA MPANZU…FADLU AFUNGUKA A-Z…AITAJA YANGA🤭🫣…

Habari za Simba leo

KOCHA wa Simba, Fadlu Davids amesikia kelele za mashabiki wanaomponda Ellie Mpanzu, kisha akamkingia kifua kwa kumtetea akisema wanambeza leo ndio watakaomshangilia baadaye, huku akiitaja Yanga kama moja ya timu zilizowafanya wakomae hadi sasa katika Ligi Kuu Bara ikiuaga mwaka 2024 ikiongoza msimamo.

Kiungo mshambuliaji huyo mpya wa Simba kutoka DR Congo, amemaliza mechi tatu za kwanza za Ligi Kuu Bara bila kufunga bao lolote wala kuasisti, licha ya kuonyesha boli lipo mguuni, lakini kocha wa kikosi hicho amevunja mkimya na kumtetea, akisema wanaombeza leo ndio watakamshangilia hapo baadaye.

Mpanzu ameshacheza mechi mbili za ugenini dhidi ya Kagera Sugar akitumika kwa dakika 57, kisha akaivaa Singida Black Stars kwa dakika 71, wakati mchezo wa nyumbani dhidi ya JKT Tanzania alitumika kwa dakika 60 ikiwa na maana ametumika jumla ya dakika 188 ndani ya mechi hizo tatu na kuanza kuzua maneno mtaani.

Hata hivyo, kocha Fadlu kumbe ameyasikia maneno hayo na kumtetea akisema, licha ya Mpanzu kushindwa kufunga au kutoa pasi ya bao bado kiwango cha winga huyo Mkongomani hakina shaka katika timu hiyo.

Fadlu alisema mchango wa Mpanzu katika mechi hizo tatu alizotumika umekuwa mkubwa ambapo amekuwa akitengeneza mashambulizi makali ambayo yalichobakiza ni kuzalisha tu mabao.

Kocha huyo alisema, mashabiki wa Simba hawatakuwa na muda mrefu kuanza kuona mambo hayo makubwa kutoka kwa winga huyo ambaye anapambana kuzoeana sawasawa na wachezaji wenzake na hata kuzoea mazingira ya ligi ya Tanzania.

“Huyu ni mchezaji aliyecheza mechi tatu pekee tangu asajiliwe, unajua kufanya mazoezi au kucheza mechi ya kirafiki ni vitu viwili tofauti na kucheza mechi ya mashindano,” alisema Fadlu na kuongeza;

“Hadi sasa ameonyesha kiwango kizuri wala hakina shaka, mabao wala hizo asisti zitakuja lakini kitu muhimu hapa kwasasa ni namna anavyoonyesha juhudi kubwa za kupambana. Amekuwa na nguvu kubwa wakati timu inatengeneza mashambulizi, ana maamuzi ya haraka katika kugeuka na kupiga mashuti kama umeona ana mashuti mengi yaliyolenga lango kuliko yale yaliyopotea, anahitaji kuzoeana zaidi na wenzake, pia kuzoea ligi ngumu ya hapa.”

Aidha Fadlu alisema sio kila mchezaji anaweza kubahatika kuzoea kwa haraka na kuonyesha kiwango kikubwa kilichokuwa kinasubiriwa.

“Soka ni mchezo unaohitaji muda niliwahi kueleza hapa kwamba wapo wachezaji waliofika muda mrefu lakini bado hawajaonyesha kitu kikubwa lakini unaona wanakuja taratibu sio kila mchezaji anaweza kuonyesha kiwango chake kwa haraka.”

AITAJA YANGA

Kocha huyo pia, alifunguka juu ya siri ya mwenendo mzuri wa timu hiyo katika Ligi Kuu hadi sasa, akisema imechangiwa kwa kiasi kikubwa na kipigo ilichopewa na Yanga katika Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Oktoba 19.

Tangu ilipofungwa katika mechi hiyo, Simba haijapoteza tena na ikiwa inauga mwaka 2024 ikiwa kileleni ikivuna pointi 40 kupitia mechi 15 na Fadlu alisema;

“Baada ya kupoteza mbele ya Yanga, kwetu haikuwa na maana kwamba tulicheza vibaya isipokuwa ni jambo la kawaida kutokea, ingawa kuanzia pale wachezaji wote walionyesha ni jinsi gani mashabiki na viongozi wanahitaji mabadiliko yao,” alisema Fadlu aliyejiunga na timu hiyo Julai 5, akichukua nafasi ya Mualgeria, Abdelhak Benchikha aliyeondoka Aprili 28, huku akiwaonya wachezaji kwamba kuwa, licha ya mafanikio hayo ila amewataka wachezaji kutobweteka akiweka wazi kazi bado ni ngumu mbele yao.

KUHUSU DUCHU

Licha ya Fadlu kufanya mabadiliko ya mara kwa mara katika kikosi hicho ila moja ya wachezaji ambao hawajacheza chini ya utawala wake ni, beki wa kulia, David Kameta ‘Duchu’ akisema ni suala la muda tu. “Ni bahati mbaya kwake kutokupata muda wa kucheza kwa sababu ya uwepo wa Shomari Kapombe na Kelvin Kijili, ila ukweli ni kwamba atacheza.”

ASHTUA MASTAA

Wakati timu hiyo ikiwasili jana jijini Dar es Salaam ikitokea Singida ilipoibuka na ushindi wa bao 1-0, lililofungwa na Fabrice Ngoma, Fadlu ameweka wazi ataweka mikakati mizuri ya kuhakikisha wachezaji wote hawatoki nje ya mipango yao.

“Tuna michezo migumu ugenini iliyokuwa mbele yetu ya kimataifa dhidi ya CS Sfaxien na Bravos do Maquis, tulifikiri tutoe mapumziko ya siku tatu hadi nne ila tunaangalia upya namna nzuri ya kuhakikisha wachezaji wanakuwa katika malengo sawia.”

PRESHA YA WAPINZANI

Moja ya mambo ambayo Fadlu amelyaona katika michezo 15 ya mzunguko wa kwanza ni presha ya wapinzani wao Yanga na Azam FC, huku akiweka wazi ilisababisha kila mchezo kuongezeka ushindani, hivyo kuongeza mvuto na msisimko wa Ligi Kuu Bara.

“Ni ngumu kuona mpinzani wako amecheza leo na akashinda huku wewe ukicheza kesho, hii ilikuwa ngumu kwa sababu kila mmoja anakuangalia, kwa hakika unapokutana na mazingira ya namna hiyo unahitaji wachezaji wakomavu kama nilionao.”

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA SPOTI XTRA JUMANNE