KIKOSI cha Simba kipo Tusinia kwa ajili ya mchezo wa nne wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi CS Sfaxien, huku kipa Moussa Camara āSpiderā akiwatoa hofu mashabiki wa Msimbazi akiwaambia wasihofu, licha ya kujua mechi ya leo Jumapili ni ngumu, lakini wanaitaka heshima ugenini.
Camara ambaye ni nguzo ya timu hiyo katika milingoti mitatu ya lango, watakuwa wageni wa CS Sfaxien Jumapili, huku wakiwa na kumbukumbu ya kuwafumua mabao 2-1 Dar es Salaam katika mechi iliyomalizika kwa vurugu zilizosababishwa na wageni na kupokewa na wenyeji waliongāoa viti Kwa Mkapa.
Msafara wa Simba uliondoka nchini, huku Camara pamoja na kocha mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids wakituma salamu mapema wakiahidi mambo matamu licha ya ugumu wa mchezo ambao hautakuwa na mashabiki kutokana na wenyeji kuadhibiwa na CAF kwa fujo walizofanya dhidi ya CS Constantine ya Algeria.
Baada ya kufika Tunisia, Fadlu alisema wapinzani wao wanawajua ndani – nje na hakuna wanachohofia, lakini Camara akasema utakuwa mchezo wa kusaka heshima na kuwatoa hofu mashabiki na wapenzi wa Simba waliopo nyumbani.
Hiyo ni mechi ya nne kwa timu zote, huku Simba ikishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi sita kama ilizonazo CS Constantine na Bravos do Maquis ya Angola zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, wakati Sfaxien ikiburuza mkia kundini ikiwa haina pointi, ikipoteza zote tatu za awali ikiwamo dhidi ya Simba.
Fadlu alisema hawajaenda Tunisia kuzuia, isipokuwa kucheza kwa kusaka ushindi ambao utawafanya wakusanye pointi zitakazowaweka pazuri katika Kundi A ili kuvuka kwenda robo fainali.
Alisema anachotaka ni wapinzani wasipate kitu kwa sababu walishawachapa nyumbani na wanataka kufanya hivyo kwao bila kujali ugumu ulipo. āNaijua Sfaxien na aina ya soka inalocheza ikiwa nyumbani tulipata alama tatu, na ugenini ni vivyo hivyo ili kukamilisha hesabu nzuri kwenye kundi. Wachezaji wote wako timamu na tayari nimeshawaambia kuwa jambo muhimu ni alama tatu tu, ili kuipa heshima timu na kuwa nafasi nzuri,ā alisema Fadlu, huku Camara akikoleza kwa kusisitiza mashabiki wa Simba hawapaswi kuwa na wasiwasi.
Kipa huyo alisema licha ya kucheza ugenini na mechi kuonekana kuwa ngumu, kiu ya kila mmoja kikosini ni kurekebisha mambo na kupata heshima kwa kushinda.
āHapa Tunisia tunataka heshima kwa kutafuta ushindi wa kwanza ugenini, kwani timu yetu imeimarika sana na kila mmoja anaridhishwa na namna maandalizi ya mchezo huo yalivyo,ā alisema Camara maarufu kama Pinpin au Spider ambaye anaongoza kwa clean sheet katika Ligi Kuu Bara akiwa nazo 12 katika michezo 15.
Msimu huu Simba ilianza mechi za ugenini kwa suluhu dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya na mchezo wa raundi ya pili uliowavusha kuingia makundi ikashinda 3-1 nyumbani, kisha ikalala 2-0 mbele ya CS Constantine katika makundi, huku ikiwa nyumbani ikishinda dhidi ya Bravos na Sfaxien kwa 1-0 na 2-1 mtawalia.
Ushindi dhidi ya Sfaxien utaifanya Simba kufikisha pointi tisa na kusikilizia matokeo ya Bravos dhidi ya CS Constantine ambazo itarudiana nazo katika mechi mbili mfululizo zijazo za kundi hilo, ikisaka tiketi ya robo fainali kwa msimu wa sita kati ya saba ya ushiriki wake wa michuano ya klabu ya CAF tangu 2018-2019.