Home Habari za michezo BAADA YA KUMALIZANA NA AL HILAL….YANGA WAANZA ‘USHUSHU’ KWA WAALGERIA😁😁😁…

BAADA YA KUMALIZANA NA AL HILAL….YANGA WAANZA ‘USHUSHU’ KWA WAALGERIA😁😁😁…

Habari za Yanga leo

BAADA ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Al Hilal Omdurman ya Sudan uliochezwa Uwanja wa De la Capitale, jijini Nouakchott, nchini Mauritania juzi usiku, Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, amesema kazi iliyobaki ni moja tu kushinda mchezo wa mwisho dhidi ya MC Alger ya Algeria, akisema kazi ya kuisoma kuifanyia ushushushu timu hiyo, imeanza mara moja.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo, ambao Yanga ilipata bao pekee kupitia kwa kiungo mshambuliaji wake raia wa Burkina Faso, Stephane Aziz Ki, Ramovic, alisema kwa sababu mchezo huo ni lazima washinde ili kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutoka Kundi A, mara moja wameanza kuifuatia MC Alger staili yao ya uchezaji, vitu mbalimbali vya kiufundi, tabia zao, na hasa wanapocheza wakiwa ugenini.

“Tunaendelea kuwasoma MC Alger ili tujue jinsi gani ya kukabiliana nao, tumekuwa tukiangalia mambo mbalimbali ya kiufundi, mfumo wao, staili ya uchezaji, na tutakapofika nyumbani tutaanza kufanya mazoezi ya kile ambacho tumekifanyia kazi,” alisema kocha huyo raia wa Ujerumani.

Alisema mchezo wa juzi ulikuwa mgumu na wenye presha kubwa kwao, lakini kwa bahati nzuri wakaibuka kuwa washindi.

“Haikuwa mechi rahisi, lakini tumeweza, nawapongeza wachezaji wangu na viongozi, ulikuwa mchezo mzuri uliokuwa na presha kubwa kwetu, umetuonesha kuwa sisi ni watu wa aina gani, tumeonesha kuwa sisi ni wapambaji.

“Tungeweza kupata bao la pili kipindi cha pili, lakini tukakosa kutumia nafasi. Sasa tunarudi Tanzania kwenye uwanja wetu kwa mchezo dhidi ya MC Alger, hautokuwa mwepesi, lakini tutapambana,” alisema kocha huyo.

Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi saba, ikiendelea kuwa nafasi ya tatu nyuma ya MC Alger ambayo ni ya pili ikiwa na pointi nane, huku kundi hilo likiongozwa na Al Hilal yenye pointi 10, na tayari imeshafuzu hatua ya robo fainali.

Mabingwa hao wa Tanzania Bara, watacheza mchezo wao wa mwisho wa hatua ya makundi Jumamosi ijayo dhidi ya MC Alger kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, saa 10:00 alasiri, ikitakiwa kushinda tu kwa idadi yoyote ya mabao ili iweze kusonga mbele.

Ikishinda itafikisha pointi 10 na kuwaacha Waalgeria hao wakisalia na pointi nane, lakini sare yoyote itaifanya kufikisha pointi nane hivyo kushindwa kufuzu kwani MC Alger itakuwa imefikisha alama tisa.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema hautokuwa mchezo rahisi kwa sababu wapinzani wao watakuja kwa nguvu ili kupata matokeo mazuri, kwani matokeo ya ushindi na sare yoyote yatawawezesha kufuzu.

“Kwetu sisi hatuna njia nyingine ya kufuzu robo fainali zaidi ya kuwagaragaza pale Benjamin Mkapa, tuko tayari kupambania hiyo heshima,” alisema Kamwe.

SOMA NA HII  KISA KOSA KOSA ZA KINA KAGERE,....KOCHA SIMBA KAAMUA KUWATOLEA UVIVU...AFUNGUKA WALICHOFANYIWA...