Home Azam FC AZAM vs YANGA….MECHI YA MAAMUZI, MABAO YA KUTOSHA….UKIBETI UHAKIKA….

AZAM vs YANGA….MECHI YA MAAMUZI, MABAO YA KUTOSHA….UKIBETI UHAKIKA….

Habari za Yanga Leo

YANGA inajivunia kuwa na wigo mpana wa kufunga mabao inapokwenda kukabiliana na Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Alhamisi hii kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar, lakini inakumbuka mara ya mwisho dimbani hapo iliondoka na maumivu makali sana.

Ukiangalia msimamo wa ligi hiyo, mabingwa watetezi Yanga wapo kileleni kwa mambo mawili, timu yenye pointi nyingi ambazo ni 64 huku pia ikifunga mabao mengi 62 ikiiacha mbali Azam yenye pointi 51 na mabao 38.

Mabao 62 yaliyofungwa na Yanga, yametokana na wachezaji 13 wanaocheza nafasi tofauti uwanjani huku eneo moja pekee ndilo bado halijahusika na bao ambalo ni kwa kipa. Yaani kuanzia eneo la beki wa kulia, kushoto, kati, kiungo mkabaji, kiungo mshambuliaji na pale mbele kwenye ushambuliaji, wachezaji wanaocheza hapo wametikisa nyavu za wapinzani msimu huu. Rekodi hiyo pia wanayo Simba, hivyo kuwa ni timu mbili tu msimu huu zilizofanya hivyo hadi sasa.

Wachezaji wa Yanga waliofunga mabao hayo ni washambuliaji Prince Dube (11), Clement Mzize (11) na Keneddy Musonda (4). Viungo washambuliaji ni Pacome Zouzoua (8), Stephane Aziz Ki (7), Maxi Nzengeli (4) na Clatous Chama(3). Viungo wakabaji ni Duke Abuya (2), Mudathir Yahya (2) na Khalid Aucho (1). Mabeki ni Ibrahim Hamad (4), Israel Mwenda (2) na Chadrack Boka (1).

Kwa upande wa Simba mabao 52 yamefungwa na wachezaji 14 ambapo washambuliaji ni Steven Mukwala (9), Leonel Ateba (8) na Valentino Mashaka (2). Viungo washambuliaji ni Jean Charles Ahoua (12), Elie Mpanzu (3), Edwin Balua (2), Awesu Awesu (2), Kibu Denis (2) na Ladaki Chasambi (1). Viungo wakabaji Fabrice Ngoma (3) na Debora Fernandes (1). Mabeki ni Shomari Kapombe (3), Mohammed Hussein (1) na Abdulrazack Hamza (1).

Azam yenye kazi kubwa kukabiliana na Yanga, katika maeneo 11 ya uwanjani, mawili tu yamekosa wachezaji waliopachika mabao ambayo ni kipa na kiungo mkabaji.

Timu hiyo imefunga mabao 38 kupitia wachezaji 11 ambapo washambuliaji ni Nassor Saadun (6), Jhonier Blanco (2) na Alassane Diao (1). Viungo washambuliaji Gibril Sillah (8), Feisal Salum (4), Idd Seleman ‘Nado’ (4) na Zidane Sereri (2). Mabeki ni Pascal Msindo (3), Lusajo Mwaikenda (3), Yoro Diaby (2) na Cheikh Sidibe (1).

VITA YA VIUNGO

Makali ya viungo katika kutengeneza nafasi na kufunga mabao yanategemewa kwa kiasi kikubwa kuamua mchezo wa Ligi Kuu baina ya Azam na Yanga itakayochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex pembeni kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, kuanzia 1:00 usiku.

Wenyeji Azam wanamtegemea zaidi kiungo mshambuliaji Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye anaingia katika mechi ya leo akiwa ndiye mchezaji wa timu hiyo aliyehusika na idadi kubwa ya mabao akifanya hivyo mara 17 akifunga matano na kutoa asisti 12.

Yanga yenyewe hapana shaka itamtegemea zaidi kiungo mshambuliaji Pacome Zouzoua pia kwani amekuwa na uwiano mzuri wa kufunga na kutoa pasi za mwisho akiwa na mabao manane na asisti nane akihusika kwenye jumla ya mabao 16 huku mshambuliaji Prince Dube aliyefunga 11 na asisti 7 akihusika na mabao 18. Wawili hao wanategemewa zaidi pale mbele.

Ukiweka kando nyota hao wawili, Maxi Nzengeli naye ana mchango mkubwa wa mabao akifunga manne na asisti nane, wakati kwa Azam FC, matumaini yao pia yapo kwa winga Gibril Sillah anayeongoza kwa ufungaji kikosini hapo akitupia kambani mara nane, akifuatiwa na mshambuliaji Nassor Saadun mwenye mabao sita.

Sillah ndiye aliwaliza Yanga katika mchezo wa duru la kwanza akifunga bao pekee wakati Azam ikishinda 1-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Rekodi zinaonyesha katika mechi kumi za mwisho kwenye ligi, moja pekee ilimalizika kwa timu hizo bila ya kufungana. Ilikuwa Juni 21, 2020 ukiwa ni msimu wa 2019-20. Zilizofuatia tisa mfululizo nyavu zimetikiswa.

Ushindi kwa Yanga katika mchezo huu utaifanya izidi kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi ambapo itafikisha pointi 67 za michezo 25 na kuendelea kuwakimbia watani wao Simba wenye pointi 57 baada ya michezo 22.

Pia ushindi huo kwa Yanga, utaifanya Azam kutokuwa na uwezo wa kumaliza ligi katika nafasi ya kwanza kwani itabakiwa na mechi nne zitakazowanyima kufikisha pointi itakazofikisha Yanga. Hivi sasa Azam ina pointi 51, ikipoteza itabakiwa na mechi nne zenye pointi 12 ambapo ikishinda zote itamaliza ligi na pointi 63.

Kwa Azam FC, ushindi utaifanya ipunguze pengo la pointi kati yake na Yanga kubaki kumi kwani itafikisha 54 pia itajihakikishia kuendelea kubaki katika nafasi ya tatu juu ya Singida Black Stars inayoifukuza kwa ukaribu kufuatia timu hiyo kuwa na pointi 50.

Wageni Yanga wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa wametoka kushinda mechi sita mfululizo za Ligi Kuu bila kuruhusu bao, mara ya mwisho ilitoka 0-0 dhidi ya JKT Tanzania Februari 10 mwaka huu.

WASIKIE MAKOCHA

Kocha Mkuu wa Azam FC, Rachid Taoussi, amesema wao kama benchi la ufundi wamefanya kazi yao kwa usahihi kilichobaki ni wachezaji kufanya kazi yao huku wakitakiwa kutorudia makosa waliyoyafanya katika mchezo uliopita walipofungwa 1-0 na Singida Black Stars.

“Tunahitaji pointi tatu, sio rahisi lakini tumejiandaa kuhakikisha tunakuwa imara, lengo ni kupata ushindi ili kurudi kwenye ushindani wa kupigania taji, hautakuwa mchezo rahisi kwasababu tunakutana na timu ambayo ilipoteza dhidi yetu, hawatakubali kupoteza tena huku na sisi tukihitaji matokeo mazuri,” amesema Taoussi.

Kocha wa Yanga, Miloud Hamdi alisema ni mchezo muhimu kwao kupata matokeo ya ushindi ili kuendelea kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutetea taji huku akibainisha kwamba ameiandaa timu yake vizuri na wachezaji wapo katika hali nzuri ya ushindani.

“Tumetoka kucheza mechi ngumu mfululizo, naamini wachezaji wangu wana uchovu lakini hilo halitaondoa hali ya wao kupambana, wataingia kwa kuwaheshimu wapinzani lengo ni kuendeleza ushindi walionao kwenye mechi sita mfululizo,” amesema Hamdi.

KUPAKI BASI

Tangu kocha Taoussi aingie nchini, Azam imekuwa ikicheza vizuri kwa kujilinda zaidi inapokabiliana na timu kubwa za Simba na Yanga.

Azam ilifunguka ikafungwa 4-1 na Yanga katika mechi ya fainali ya Ngao ya Jamii Agosti 12, 2024 na ikamfuta kazi aliyekuwa kocha wake Youssouph Dabo na ikafungwa pia 2-0 na Simba katika Ligi Kuu Septemba 26, 2024.

Tangu hapo Azam imeonekana kubadilika na kucheza kwa nidhamu sana. Ilipaki basi licha ya Yanga kubaki na wachezaji 10 uwanjani baada ya Ibrahim Bacca kutolewa kwa kadi nyekundu katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 Novemba 2, 2024.

Azam pia ikacheza kwa nidhamu kubwa na kulazimisha sare ya 2-2 dhidi ya Simba Februari 24, 2025 katika Ligi Kuu Bara, shukrani kwa bao la dakika za jiooni la mtokea benchini Zidane Sireri.

Kwa ambacho Azam imefanya katika mechi tatu zilizopita na kuzivuruga timu hizo kubwa msimu huu chini ya kocha Taoussi, ni jambo linalotarajiwa na leo kucheza kwa staili hiyo ambayo ina nafasi kubwa ya kuivuruga Yanga tena.

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA SPOTI XTRA JUMAPILI