Home Habari za michezo KUHUSU SIMBA AU YANGA…..TCHAKEI ATAJA ANAPOENDA …AFUNGUKA A-Z DILI LILIVYO…

KUHUSU SIMBA AU YANGA…..TCHAKEI ATAJA ANAPOENDA …AFUNGUKA A-Z DILI LILIVYO…

Tetesi za usajili Simba leo

UJIO wa Elvis Rupia ambaye ndiye kinara wa upachikaji wa mabao Singida Black Stars na Jonathan Sowah ni kama umemfunika Marouf Tchakei aliyekuwa anasumbua kikosini.

Kiungo huyo mshambuliaji ubora wake ulidaiwa kuziingiza vitani Simba na Yanga kuwania saini yake ambaye msimu wa kwanza alifunga mabao tisa.

Ni kiungo fundi aliyejiunga na timu hiyo mwanzoni mwa msimu uliopita, na sasa anafu-kuzia rekodi yake kwani tayari amepachika mabao matano licha ya uwepo wa wa- shambiliaji ambao wameonyesha kutumia vyema nafasi.

Tchakei aliyezaliwa Desemba 15, 1995 huko Bassar, Togo, alijiunga na Singida Black Stars akitokea AS Vita ya DR Congo kwa mkataba wa miaka miwili.  kiungo huyo amefichua mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na furaha yake ndani ya timu hiyo anayoitaja kuwa na wachezaji wengi wenye vipaji.

ISHU YA SIMBA, YANGA IKO HIVI

Dirisha kubwa la usajili lililofungwa Agosti 30, mwaka jana lilimhusisha kutua kwa watani wa jadi Simba na Yanga, lakini haikuwa hivyo na mwenyewe ameeleza ilivyokuwa. “Dirisha la usajili ni mambo mengi yanazungumzwa. Ni kweli hadi mimi nilisikia kuhusishwa na hizo timu, lakini hakukuwa na kitu chochote kilichokuwa kinaendelea. Mimi ni mali ya SBS,” anasema.

Tchakei anasema timu iliyomfuata mezani na kufanya naye mazungumzo ndio anaitumikia kwa sababu iliheshimu ubora wake na sasa anapambana kuhakikisha anaifanyia kile walichoamini atakifanya.

KUCHEZA NA RUPIA, SOWAH

Msimu uliopita kulikuwa na Bruno Gomes aliyekuwa fundi eneo la kiungo mshambuliaji akifunga mabao tisa, sasa Tchakei anasema kuna nyota wengi wanaompa ushindani na kukuza kipaji chake akifurahia uwepo wa Rupia na Sowah ambao anadai wanampunguzia majukumu.

“Rupia, Sowah ni aina ya washambuliaji ambao wana jicho la kuona goli na kiu ya kufunga ni rahisi kufanya nao kazi. Nafurahia kuongezwa kwao na nimekuwa nikicheza kwa kujiachia nikiamini nina watu wenye uwezo mkubwa kufanya kazi ya kumalizia mipira na pia wanajua kutengeneza nafasi, anasema Tchakei.

“Nafikiri kila timu inatamani kuwa na wachezaji wa aina kama zao msimu huu. Safu imechangamka ushindani ni mkubwa na kila mmoja anafanya kazi yake kwa usahihi, hili linaongeza chachu ya ushindani kikosini lakini pia kwa wapinzani.”

SINGIDA KIMATAIFA

Singida Black Stars ipo nafasi ya nne kwenye msimamo ikiachwa pointi moja na Azam FC jambo ambalo kiungo huyo linampa jeuri kuwa kwenye mechi walizobakiwa nazo wana uhakika wa kumaliza nafasi nne za juu na kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa.

“Nafasi ya tatu na nne hatung’oki. Tuna kila sababu ya kuipambania timu hii kuweza kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa. Kuhusu kombe tumepoteza matumaini mzunguko wa pili ambao tumepoteza pointi nyingi,” anasema.

“Ili kupata nafasi ya kutwaa taji la msimu ni kumfunga mpinzani wako ambaye pia anawania taji hilo. Tumelishindwa kwa kupoteza dhidi ya Yanga mechi zote mbili, dhidi ya Simba tumepoteza mchezo mmoja tuna mchezo mwingine ambao tunatakiwa kuhakikisha tunapata matokeo, lakini kwa Azam FC tumechukua pointi tatu bado tatu.”

NI DIZAINA

Ufundi anaouonyesha kwenye kikosi cha Singida ukiambatana na unyumbulifu wake akiwa na mpira mguuni na mashuti makali ambayo ni kero kwa makipa hilo kwake anadai ni ziada tu kwani alikuwa na ndoto ya kuwa msanifu kurasa kabla ya mpira kuchukua nafasi.

“Ndoto yangu ilikuwa ni kuwa msanifu kurasa bora zaidi na kipaji hicho kilionekana mapema nikiwa na umri mdogo na nilifanikiwa kuingia darasani kwa ajili ya hilo.

“Baadaye baada ya akili kukomaa soka likaniteka akili nikaamua kujikita huko, lakini mimi ni dizaina ambaye nimeingia darasani na kusomea nina cheti siku ikitokea nikaamua kuachana na soka nitaendeleza ndoto yangu ya kuwa mbunifu mkubwa.” anasema.

AKAMINKO, FEI BALAA

Singida imekutana na Azam FC mara mbili msimu huu wakigawana pointi tatu – tatu kwa kila timu kushinda mchezo wake wakianza Azam FC kushinda mabao 2-1 na mzunguko wa pili Singida wakashinda bao 1-0 mechi ambazo zimempa nafasi Tchakei kubaini ubora wa James Akaminko.

“Ni msimu wangu wa pili kucheza ligi ya Tanzania. Ni nchi ambayo ukiondoa wachezaji wa kigeni pia wana vipaji vikubwa vya wachezaji wazawa, lakini naweza kusema wachezaji wa Azam FC wanaocheza eneo la kiungo ni wazuri sana. Wamenipa shida tulipokutana nao kwenye michezo yetu miwili tuliyocheza,” anasema.

“James Akaminko, Feisal Salum na wengine wanaocheza eneo la kiungo siwezi kuwataja kwa majina ni wachezaji wazuri na wana muunganiko mzuri kwenye kikosi chao.”

SIO 10 TU HATA SABA

Mbali na kuwa na uwezo mkubwa wa kucheza nyuma ya mshambuliaji au ‘mshambuliaji wa uongo’, Tchakei anaweza kushambulia akitokea pembeni hasa kulia.

Eneo lingine analoweza kucheza ni kiungo mkabaji na hapa unaweza usipate ubora wake kwani kucheza kwake chini kutamnyima uhuru wa kuwa karibu na eneo la hatari la wapinzani. “Kabla sijakubalika zaidi kwenye eneo la kiungo mshambuliaji nilianza kutumika pembeni na nafiti vizuri eneo hilo, lakini napenda zaidi kucheza namba kumi. .” anasema.

KUPANDA NDEGE

Kuna baadhi ya wachezaji licha ya vipaji vikubwa na kuaminiwa ni ngumu kusafiri nao kwa ndege na hilo pia lipo kwa Tchakei. “Nimekuwa nikipata nafasi mara kwa mara ya kusafiri kwa anga, lakini sio rahisi kwani bado sijapata ujasiri huo, hivyo kabla ya kuondoka ni lazima nifanye sala… muda wa kupanda ndege ukifika ni lazima nitafanya sala kwa ajili ya kukabidhi ndege yetu kwa Mungu.”

Credit:- MwanaSpoti

SOMA NA HII  HII HAPA 'VITA' YA KIMYA KIMYA KATI YA TSHABALALA NA YAO KOUASSI ....MAMBO NI 🔥🔥🔥....