OFISA Habari wa Klabu ya Yanga, Ali Kamwe, ameonya mashabiki wa timu hiyo dhidi ya kushangilia mapema ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, akisema kuwa bado kuna kibarua kigumu katika michezo mitatu iliyosalia.
Yanga, ambao wako kileleni mwa msimamo wa ligi, wamebakiza mechi tatu za mwisho dhidi ya Namungo FC, Tanzania Prisons, na Dodoma Jiji FC. Mechi ya mwisho itachezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, uliopo Mwenge, jijini Dar es Salaam.
Kamwe amesema mashabiki wanapaswa kuelewa kuwa licha ya timu kuonekana kuwa na nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa, bado hawajafika walipokusudia na wanahitaji umakini mkubwa.
“Mechi hizi tatu ni ngumu sana. Hata kama unaweza kuziangalia kwa jicho la kawaida na kuziona rahisi, ukweli ni kwamba kila mpinzani anapambana kuokoa alama. Huu ni wakati wa mapambano ya kweli,” amesema Kamwe.
Ameongeza kuwa kila hatua ni muhimu na mashabiki waendelee kuiunga mkono timu yao kwa utulivu, huku wakitambua kuwa wapinzani wao wana nia kubwa ya kuwazuia.
“Ni vita ya kweli. Kila upande unataka ushindi. Mikono mingi ipo kwa ajili ya kutuangusha, hivyo ni wakati wa kuwa makini zaidi,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Yanga imeelekea visiwani Zanzibar kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Muungano, itakayopigwa Aprili 23 na 25, ambapo wanatarajiwa kumenyana na KVZ kutoka visiwani humo.
Kamwe amesema maandalizi hayo ni sehemu ya kuhakikisha wachezaji wanabaki katika hali nzuri ya ushindani huku wakikamilisha msimu kwa mafanikio.