KIUNGO mahiri wa Klabu ya Yanga, Clatous Chama, bado hajajua hatma yake ya kuendelea kusalia Jangwani kwa msimu ujao wa 2025/26, huku suala hilo likielekezwa moja kwa moja mikononi mwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hamdi Miloud.
Chama, ambaye alijiunga na Yanga kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea kwa watani wao wa jadi Simba , anatarajiwa kumaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu huu. Kwa sasa, hakuna maamuzi rasmi yaliyotolewa kuhusu kuongeza mkataba huo.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amethibitisha kuwa nyota huyo wa Zambia alisaini kandarasi ya muda mfupi, na maamuzi ya hatma yake kwa msimu ujao yatategemea mapendekezo ya kocha Miloud.
“Hakuna mtu asiyejua kuwa mkataba wa Chama ulikuwa wa mwaka mmoja na sasa unaelekea ukingoni. Kuhusu kuongeza mkataba mwingine, hilo lipo kwa kocha Hamdi katika mapendekezo yake kwa msimu ujao,” amesema Kamwe.
Ameongeza kuwa hadi sasa bado hawajapokea taarifa rasmi kutoka kwa kocha huyo kuhusu iwapo Chama ataendelea kuwa sehemu ya kikosi cha Yanga msimu ujao, lakini anaamini ubora wa kiungo huyo ni jambo lisilo na mjadala.
“Kila mmoja anatambua ubora wa Chama. Nina imani suala la kubaki au kuondoka lipo kwa kocha wetu, kulingana na mipango na mahitaji ya kikosi chake kwa msimu wa mashindano ujao,” amesema.
Mashabiki wa Yanga sasa wanasubiri kwa hamu kuona kama kocha Hamdi ataamua kumbakisha Chama ambaye amekuwa na mchango mkubwa tangu alipojiunga na timu hiyo.