Home Habari za michezo KISA UKIMYA MWINGI….SIMBA WAIBUKA NA HILI JIPYA….ISHU YA FADLU KUSEPA HII HAPA…

KISA UKIMYA MWINGI….SIMBA WAIBUKA NA HILI JIPYA….ISHU YA FADLU KUSEPA HII HAPA…

Habari za Simba

KLABU ya Simba imesema kwa sasa viongozi wake wa ngazi ya juu wamekuwa na vikao kila siku kwa ajili ya usajili na kupanga mikakati kabambe kwa ajili ya msimu ujao, huku ikithibitisha rasmi kuwa imembakisha Kocha Mkuu, Fadlu Davids kwa msimu mwingine ujao na kukikiri haikuwa rahisi hata kidogo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, amewaambia wanachama na mashabiki wa Simba kuwa wasione wapo kimya wakadhani labda hakuna kitu kinachofanyika, badala yake viongozi wa klabu hiyo wamekuwa na vikao vya kila siku kuhakikisha mambo yanakwenda, hasa kwenye usajili ambao wanaendelea nao, pamoja na mikakati mingine ya klabu ambayo kwa sasa ni siri hadi pale watakapoamua kuyaanika hadharani.

“Hatupo kimya hata kidogo kama wengi wanavyodhani, vikao vinaendelea kwa viongozi wa Simba pamoja na Fadlu kuhusu usajili ambao tunaendelea nao na mikakati mingine mingi, tukishamaliza mambo ya ndani kila kitu kikishakaa kwenye eneo lake, baada ya hapo tutakuja nje kuwaeleza watu mwelekeo wetu ni upi.

“Niwaambie tu Wanasimba kuwa hakuna siku inayopita bila viongozi wa juu wa Simba kufanya vikao kujadili mustakabali wa klabu na maandalizi ya msimu ujao.

“Hivi karibuni tutaanza kutoa, ‘thank you’ kwa wachezaji waliomaliza mikataba na hatuwahitaji, baada ya hapo tutakuja kuwatangazia wachezaji tunaoendelea nao, tukimaliza tutaanza kuwakaribisha wachezaji wapya, tukiondoka hapo tunakwenda ‘pre seasons’ kabla ya Tamasha la Simba Day, halafu tunakwenda kwenye Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Ahmed.

Alithibitisha rasmi kuwa kocha huyo amesaini mkataba mwingine na kuamua kubaki na klabu hiyo, akikiri kuwa klabu mbalimbali kubwa zilikuwa zinamhitaji, lakini wamepambana mno kumbakisha, huku mwenyewe akionekana kuipenda Simba.

“Si timu za Afrika tu, hata barani Ulaya alikuwa na ofa, timu zilikuwa zinamhitaji kutokana na ubora aliouonesha hapa Afrika hasa akiwa kwetu, sasa vikumbo vilikuwa vikubwa kweli kweli, klabu zilikuwa zinahitaji saini ya Fadlu.

“Nikwambie ni klabu kubwa kubwa barani Afrika, lakini mwenyewe ameshafanya maamuzi sahihi kwa maslahi yake, nayo ni kubaki Simba, kwa msimu mwingine unaokuja, ameshafanya hilo, ameshaamua hivyo kwa sasa anashirikiana na viongozi kwa ajili ya kuboresha timu,” alisema.

Fadlu, raia wa Afrika Kusini, alijiunga na Simba akitokea Raja Casablanca alipokuwa kocha msaidizi, lakini alipewa mikoba wa kuwa Kocha Mkuu Msimbazi.

Amekuwa kipenzi wa mashabiki wa Simba kutokana na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho kwa mara ya kwanza tangu 1993, ambapo kwa misimu kadhaa ya hivi karibuni ilikuwa inaishia robo fainali ya michuano ya kimataifa.

SOMA NA HII  UONGOZI SIMBA WAKUBALI YAISHE KWA MIQUISSONE...VIGEZO VYA AL ALHY KUMRUHUSU ARUDI VYAWATISHA...