Home Habari za michezo BAADA ATEBA KUUZWA SIMBA…EDO KUMWEMBE ATUPA DONGO KWA FADLU….

BAADA ATEBA KUUZWA SIMBA…EDO KUMWEMBE ATUPA DONGO KWA FADLU….

Habari za Simba leo

LEONEL Ateba amepewa ‘thank you’ pale Msimbazi. Simba wamepata sehemu nzuri ya kutokea kwa Ateba. Hawana lawama naye kwa sababu wamemuuza kwenda katika klabu ya Al-Shorta ya Irak. Mabosi wa Simba watakuwa wanatabasamu pindi wanapotazama muamala wa Waarabu ulioingia kwenye klabu yao.

Ndani ya mioyo ya mashabiki, wanachama na viongozi ni wazi kwamba Ateba alipaswa kuwa mchezaji wa kupisha njia aje mshambuliaji mwingine mwenye makali zaidi yake. Hili lilikuwa katika tafakuri zao hata kabla Simba hajaipokea ofa kutoka Ghuba ya Uajemi.

Kwamba hawakuvunja mkataba wake na ndio kwanza wakapata pesa kupitia yeye, basi hiyo ni bonasi kubwa kwao. Ni kama zali tu kwa mchezaji wa aina ya Ateba. Haukuwa uwekezaji mzuri. Ilitazamiwa Simba wapate hasara kwa kumlipa fidia ya kuvunja mkataba, lakini ndio kwanza wamepata pesa.

Naambiwa kwamba Ateba alikuwa chaguo la kwanza la kocha mbele ya Steve Mukwala ingawa ukweli ni kwamba Mukwala alionekana kuwakosha wengi kuliko Ateba. Mukwala alicheza kwa dakika chache zaidi kuliko Ateba, lakini alifunga mabao ya kutosha.

Wakati Ateba alionekana kuwa mzito, Mukwala alionekana mwepesi na msumbufu katika eneo la mwisho kuliko Ateba. Hata hivyo mara nyingi chaguo la kwanza la Fadlu Davis lilikuwa Ateba kuliko Mukwala kitu ambacho baadaye mabosi wa Simba walianza kumgeuzia kibao kocha wao.

Vyovyote ilivyo Simba waliendelea kurudi nyuma katika makali ya safu yao ya ushambuliaji kulinganisha wakati ule walipokuwa na kina John Bocco, Chris Mugalu na Meddie Kagere. Ateba na hata Mukwala hawajawahi kufikia makali yao.

Furaha ya viongozi wa Simba kupata pesa katika dili la Ateba inakamilishwa na ukweli kwamba tayari katika akiba wana mshambuliaji hatari ambaye anawahakikishia mabao. Jonathan Sowah. Huyu anaweza kuwa mshambuliaji hatari zaidi ambaye wamewahi kumpata tangu walipoondoka kina Bocco.

Huyu ndiye mchezaji ambaye hata mashabiki wa Simba wana uhakika naye kwa sababu walimuona makali yake akiwa na Singida Big Stars. Ndani ya miezi sita tu alikuwa amefunga mabao ya kutosha kuliko hata washambuliaji walioanza ligi mwanzoni mwa msimu.

Furaha ya mabosi wa Simba inaweza kuwa kubwa zaidi pindi wanapokumbuka kwamba hawakupata hasara ya kuvunja mkataba wa Ateba. Alikuwa bado ana mkataba na walilazimika kwenda naye Misri katika maandalizi ya msimu mpya. Kuachana na Ateba bila ya kuvunja mkataba ni dili zuri.

Klabu zetu kubwa zimekuwa zikiingia hasara za kimyakimya kwa kuvunja mikataba ya wachezaji wapya kila kukicha. Wakati mwingine siri zinafichuka tunaposikia kuwa wamefungiwa kusajili na Fifa baada ya kushindwa kulipa fidia za mikataba za wachezaji hawa.

Hapo hapo kuna jambo la kujifunza. Simba waendelee kuwa makini katika masuala ya usajili. Warudi katika ramani ile ile waliyokuwa wanaitumia zamani kuwapata kina Clatous Chotta Chama, Luis Miquissone, Meddie Kagere na wengineo.

Miaka ya karibuni Simba wamekosea zaidi kuliko watani zao – Yanga. Mfano ni huyu huyu Ateba. Sidhani kama alikuwa mshambuliaji wa kuivusha Simba kwenda katika hatua ya juu zaidi baada ya miaka ya karibuni kufika robo fainali za CAF mfululizo.

Walihitajika wachezaji wakali zaidi ambao wangeivusha Simba kutoka hatua ya robo fainali kwenda mbele zaidi. Matokeo yake walisajiliwa wachezaji wengi ambao waliirudisha timu nyuma. Hata katika ligi ya ndani haishangazi kuona mtani akitawala zaidi kwa sababu hesabu zake za usajili anapatia zaidi kuliko kukosea. Sio kwamba watani hawakosei, hapana. Huwa wanakosea lakini wanapatia zaidi.

Haishangazi kuona kila siku Simba wanalalamika kwamba wanajenga kikosi upya. Ateba anaweza kuwa mchezaji wa tano kuondoka klabuni baada ya kufika miezi 12 tu iliyopita. Na anaondoka huku mabosi wakiwa hawana lawama yoyote kutoka kwa mashabiki.

Kuna mambo mawili ambayo mabosi wa Simba pia wanapaswa kujifunza katika hili la Ateba. Kwanza kabisa kuangalia mwenendo wa mchezaji huko alikotoka. Kama kuna klabu ilivunja mkataba wake miezi michache baada ya kuwasili kwake, basi lazima kuna walakini kwa mchezaji mwenyewe. Hakuna timu ambayo haitaki kukaa na mchezaji mzuri.

Kwa mujibu wa Wikipedia, Ateba aliichezea USM Alger mechi 12 tu. Ukifika hapo lazima ujiulize zaidi na zaidi. Haikuwa bahati mbaya. Lazima kulikuwa na walakini ambao Simba walipaswa kuujua kabla ya kumpa mkataba.

Kitu kingine ambacho Simba na watani zao wanapaswa kukiangalia kwa umakini siku hizi ni hii sifa ya mchezaji kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa. Wakati mwingine mawakala wa mchezaji huwa wanacheza dili na makocha wa timu za taifa wawaite wachezaji wao ili watengeneze wasifu zaidi.

Kuna mawakala wanatoa pesa kwa makocha wawaite wachezaji wao katika vikosi vya timu za taifa kule Afrika Magharibi kwa ajili ya kutengeneza wasifu bora. Hata hivyo, wachezaji hawa wanakuwa na viwango vya kawaida. Sisi ambacho tutaangalia kwa haraka ni kwamba mchezaji ni mkali kiasi kwamba aliwahi kuitwa kikosi cha timu ya taifa ya Cameroon au Ghana. Kumbe mchezaji ni wa kawaida tu.

Na sasa kuna uwezekano mkubwa pia kikosi cha kwanza cha Simba ambacho kitacheza na mtani Septemba 16 katika pambano la Ngao ya Jamii kitakuwa na wachezaji kama tisa wapya watakaoanza siku hiyo. Mashabiki wataona wazi kwamba timu yao inaundwa upya.

Pole kwa Fadlu ni kwamba safari hii hatapewa muda licha ya kwamba atakuwa na kikosi kipya. Afrika huwa hatuna utamaduni wa kuwapa makocha muda. Tunachoangalia kwa haraka haraka ni ukali wa kikosi na sio mambo ya muda.

Credit:- MwanaSpoti/Edo Kumwembe

SOMA NA HII  BADO DAKIKA KIDUCHU TUUU...DUNIA NZIMA KWA MKAPA...MZEE WENGER MAPEMA TU NA KOTI LAKE...