Home Habari za michezo MMADAGASCA AFICHUA ALIVYOICHOMOLEA SIMBA ATUE YANGA….ATAJA WACHEZAJI WAPYA…

MMADAGASCA AFICHUA ALIVYOICHOMOLEA SIMBA ATUE YANGA….ATAJA WACHEZAJI WAPYA…

Habari za Yanga leo

LICHA ya kwamba Yanga haijathibitisha kumchukua Romuald Rakotondrabe kuwa kocha mkuu wa timu hiyo, lakini mwenyewe amefichua namna alivyokubali dili alilopewa na kuichomolea Simba.

Kwa siku za karibuni, kumekuwa na taarifa za Yanga kuwa hatua za mwisho kusitisha mkataba wa Kocha Romain Folz, baada ya kuwepo shinikizo la kufanya hivyo kutoka kwa mashabiki wakionyesha kutoridhishwa na mbinu zake za ufundishaji.

Katika mahojiano maalum na Jarida la L’Express de Madagascar, Kocha Romuald Rakotondrabe maarufu kwa jina la Rôrô, amesema baada ya kufanya vizuri na Madagascar kwenye michuano ya CHAN 2024 timu hiyo ikimaliza nafasi ya pili ilipopoteza fainali kwa kufungwa mabao 3-2 na Morocco, klabu mbalimbali zikavutiwa naye ikiwemo Al Merreikh ya Sudan na Simba SC, ambao ni watani wa jadi wa Yanga.

Akianza kuzungumzia dili alilikataa kutoka kwa Al Merreikh, Rôrô amesema: “Nilisita kwa sababu sikuwa nimevutiwa sana, hasa kwa kuwa klabu hiyo (Al Merreikh) inacheza mechi zake nje ya nchi.”

Mbali na Wasudan hao ambao msimu uliopita walicheza Ligi ya Mauritania sambamba na ndugu zao Al Hilal kufuatia nchini kwao kuwa na machafuko, pia Klabu ya Simba ilionesha nia ya kumuhitaji Rôrô.

Inafahamika kuwa Simba ilimfuata kocha huyo siku chache baada ya Fadlu Davids kuaga na kuiacha timu hiyo ikipambana kuziba pengo lake huku ikikabiliwa na mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United na mbili za Ligi Kuu Bara.

“Klabu ya Simba pia ilionesha nia, lakini nimeridhishwa zaidi na mipango na malengo ya Yanga.

“Viongozi wa klabu (Yanga) wana dhamira ya kufika mbali zaidi katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Wamenihakikishia kuwa klabu ina kila kitu kinachohitajika kufikia malengo yake, wachezaji wenye ubora, ari, na wanaothaminiwa. Na pia nitaruhusiwa kusajili wachezaji wapya pale itakapohitajika,” amesema kocha huyo akisisitiza pia Yanga imempa nafasi ya kuja na watu wake wa benchi la ufundi.

Ikumbukwe kuwa, wakati Simba ikimsaka mrithi wa Fadlu kabla ya kumtangaza kocha raia wa Bulgaria, Dimitir Pantev aliyetokea Gaborone United, alikabidhiwa kikosi hicho Hemed Suleiman ‘Morocco’ kwa mechi moja ya marudiano ya kimataifa, huku Seleman Matola akiiongoza mechi mbili za Ligi Kuu Bara.

Hata hivyo, Simba wakati inamsaka mrithi wa Fadlu, iliweka masharti ya kuja ajaye asiye na lundo la wasaidizi kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake ndio maana Pantev amekuja na msaidizi mmoja pekee, Simeonov Boyko Kamenov.

Fadlu alipotua Simba, alikuja na wasaidizi wake ambao ni Darian Wilken (Kocha Msaidizi), Wayn Sandilands (Kocha wa Makipa), Durell Butler (Kocha wa Utimamu) na Mueez Kajee (Mchambuzi wa Video) ambapo pia ameondoka nao kuelekea Raja Casablanca ya Morocco.

Kitendo cha Rôrô kuhakikishiwa na Yanga anaweza kuja na wasaidizi wake wa benchi la ufundi, moja kwa moja akashawishika kusaini tofauti na Simba iliyoweka masharti ya kocha ajaye asiwe na wasaidizi wengi.

Rôrô anaondoka Madagascar baada ya kuiongoza timu hiyo kumaliza nafasi ya pili katika mashindano ya CHAN 2024, ambapo timu hiyo ilicheza mechi saba, ilifunga mabao tisa na kuruhusu saba ikiwa na cleansheet mbili pekee. Ilipoteza mechi ya fainali dhidi ya Morocco kwa mabao 3-2.

KUHUSU FOLZ

Kwa upande wa Folz, alitambulishwa ndani ya Yanga Julai 14, 2025, tayari ameiongoza timu hiyo kwenye mechi tano za mashindano, akishinda nne na sare moja huku akiivusha kwenda hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika mechi hizo tano, Yanga imefunga mabao tisa, haijaruhusu nyavu zake kutikiswa ikimaanisha ina clean sheet tano. Pia Yanga chini ya Folz imetwaa taji moja la Ngao ya Jamii kwa kuifunga Simba bao 1-0.

Taarifa zinasema kocha huyo Mfaransa anaondoka si kwa sababu ya matokeo mabaya, bali mashabiki hawamuelewi mbini zake za ufundishaji kwani timu inashinda bila kutoa burudani, hivyo wametoa shinikizo lililopenya kwa uongozi na kufikia uamuzi wa kumsitishia mkataba wake.

Credit:- MwanaSpoti.

SOMA NA HII  JULIO :- MAYELE KIKWETU NI POMBE ...MAANA YAKE KASHALEWA..ATATUFUNGAJE ..?...TUSHINDANE UWANJANI...