Home Azam FC IBENGE ALIOMBEA MUDA ‘PISHI LAKE’ AZAM FC….

IBENGE ALIOMBEA MUDA ‘PISHI LAKE’ AZAM FC….

Habari za Azam FC

KOCHA Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge amesema bado wachezaji wanaendelea kuzisoma falsafa zake, lakini anaamini kadri muda unavyokwenda watakuwa bora zaidi na wenye ushindani wa hali ya juu.

Ibenge aliyejiunga na Azam msimu huu akiwa amesimamia mechi mbili za Ligi Kuu Bara, huku akiweka rekodi ya sare na kufunga mara moja katika kila mchezo, alitua kikosini hapo akitokea Al Hilal ya Sudan iliyoweka maskani ya muda nchini Mauritania.

Kocha huyo alisema anahitaji kuona wachezaji wa timu hiyo wakifika kiwango cha kujihakikishia ushindi kila wanapokuwa uwanjani.

Alisema kuwa kwa sababu hicho ni kikosi kipya kwake na wachezaji wanahitaji muda zaidi wa kushika falsafa zake vyema, kwa sasa ni suala la muda tu kwani kila kitu kitakuwa sawa.

“Muda utafika wa kuona kile ninachokitengeneza kwa wachezaji, kwani nahitaji kiwe juu na kila tunapokuwa na majukumu ya mechi ushindi unakuwa ni uhakika,” alisema Ibenge na kuongeza:

“Sina maana kwamba sijaona ushindani wa Ligi Kuu ama michuano ya CAF, isipokuwa kila kocha ana mpango wake wa kuhakikisha anatimiza malengo ya klabu anayoitumikia.”

Ibenge aliongeza kuwa, “sitamani kuona timu inafungwa au kupata sare kama ilivyokuwa dhidi ya JK Tanzania, kitu ambacho nakifanyia maboresho ya hali ya juu kwa sasa.

“Malengo ya klabu ya Azam ni makubwa ndiyo maana kila mchezaji mbali na mbinu ninazozifundisha pia nawajenga kujua majukumu yao. Wakiyafanya kwa ufasaha watakuwa na thamani kubwa sokoni,” alisema Ibenge.

Azam mpaka sasa imecheza mechi mbili, huku ikiifunga Mbeya City mabao 2-0 na JKT Tanzania sare ya 1-1.

SOMA NA HII  KIBU DENIS APIGWA KO NA SIMBA...MBADALA WAKE WAANZA KUVUNJA REKODI ZAKE HIZI