Baada ya uongozi wa klabu ya Simba kufikia makubaliano ya kumfuta Meneja Dimitar Pantev, klabu hiyo inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, imeanza harakati za kusaka mrithi wa kubeba mikoba yake.
Simba impoteza mechi mbili za mwanzo ilizocheza kwenye kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo, ilianza kufungwa nyumbani kwa bao 1-0 na Petro Luanda ya Angola kisha ikafungwa ugenini na Stade Malien ya Mali kwa mabao 2-1.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kushika mkia katika msimamo wa kundi D linaloongozwa na Petro yenye pointi nne sawa na Stade Malien huku Esperance ya Tunisia ikiwa nafasi ya tatu na pointi mbili.
Awali, iliripotiwa kuwa uongozi wa Simba ulimpa Pantev mechi kadhaa za kurekebisha hali ya mambo kwa timu yao vinginevyo itamfuta jambo ambalo tayari wamelitekeleza mapema jana baada ya mfululizo wa vikao vya mabosi wa klabu hiyo.
Mbali na matokeo yasiyoridhisha, uongozi wa Simba pia unaripotiwa haufurahishwi na upangaji wa kikosi wa Pantev ambao, unaamini ndio chanzo cha timu yao kutokuwa na muelekeo mzuri.
Kwa sasa kuna makocha watano ambao kwa wasifu wao, wanaonekana ni watu wanaoweza kuwa sahihi kuisimamia timu hiyo na kuipa mafanikio.
Uzoefu wa kufundisha soka la Afrika, mbinu na nguvu ya ushawishi, ni sababu ambazo zinawafanya makocha hao kuwa na daraja la kupewa jahazi la kuiongoza Simba na ikakaa kwenye mstari ndani ya muda mfupi.
Baadhi ya makocha hao, kwa nyakati tofauti walionyesha hamu ya kuinoa Simba na kufundisha nchini Tanzania.
MONDHER KEBAIER
Wakati Simba inasaka Kocha mpya kabla ya msimu wa 2024/2025, Kocha Raia wa Tunisia mwenye umri wa miaka 55, Mondher Kebaier ni miongoni mwa makocha walioonyesha nia ya kuinoa Simba ingawa uongozi wa klabu hiyo uliamua kumchukua Fadlu Davids.
Kebaier ambaye ana leseni Daraja A ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), ni muumini wa mfumo wa 4-3-3 na ana uzoefu na mafanikio makubwa ya soka la Afrika ambalo amelifundisha kwa miaka 25 sasa.
Amefundisha klabu nane tofauti ambazo ni AS Djerba, CA Bizertin, AS Kaserine, Etoile Du Sahel, Club Africain, AS Marsa, Esperance na Raja Casablanca na ameifundisha pia timu moja ya Taifa ambayo ni ya Tunisia.
Mwaka 2013 alitwaa Kombe la Tunisia akiwa na CA Bizertin.
MILUTIN SREDOJEVIC ‘MICHO’
Kocha huyo Mserbia ni miongoni mwa makocha wakubwa na walioweka thamani ya juu katika soka la Afrika kutokana na uzoefu wa kufundisha kwa muda mrefu idadi kubwa ya klabu za soka na timu za Taifa Barani humu.
Ana Uzeofu wa soka la Tanzania kwa vile aliwahi kuifundisha Yanga hapo nyuma lakini klabu nyingine za Afrika alizowahi kuzifundisha ni SC Villa, St. George, Orlando Pirates, Al Hilal, Al Merrikh na sasa anainoa ES Setif.
Amewahi kuzifundisha timu za taifa za Zambia, Rwanda, Uganda na Libya kwa nyakati tofauti na akiwa na umri wa miaka 56 hivi sasa, Micho ana leseni ya juu ya Uefa (Pro Licence) ambayo inamuwezesha kufundisha timu yoyote Afrika.
Katika miaka 23 aliyofundisha Afrika ametwaa jumla ya mataji 15 ambapo 14 ni ya klabu na moja ni la timu ya taifa.
HUBERT VELUD
Kwa sasa hana timu tangu alipoachana na AS FAR, Februari 5 mwaka huu na anamiliki leseni ya UEFA Pro License.
Velud ambaye ni Raia wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 66, anapendelea mfumo wa 4-2-3-1 na amefundisha Afrika kwa miaka 16.
Timu za Taifa za Afrika alizowahi kuzinoa ni Togo, Sudan na Burkina Faso na klabu alizozinoa ni Hassania Agadir, ES Setif, CS Constantine, USM Alger, TP Mazembe, Difaa El Jadida, JS Kabylie na FAR Rabat.
Ametwaa idadi ya mataji nane katika miaka hiyo 16 aliyofundisha ndani ya ardhi ya Afrika.
JOHNATHAN MCKINSTRY
Kwa sasa anaifundisha timu ya Taifa ya Gambia lakini amekuwa hana maelewano mazuri na uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini humo.
Mahusiano duni baina ya McKinstry na Gambia, yanaweza kutumiwa vyema na Simba kumshawishi kocha huyo raia wa Ireland Kaskazini.
McKinstry mwenye leseni ya Juu ya Ukocha ya Uefa, anapendelea mfumo wa 4-2-3-1 akipenda zaidi soka la kushambulia.
Kwa ngazi ya Klabu ametwaa mataji matatu akiwa na Gor Mahia ya Kenya na ametwaa taji moja akiwa na timu ya Taifa ya Uganda.
Amewahi kufundisha pia timu ya taifa ya Rwanda.
NASREDDINE NABI
Huenda ikawa sio rahisi kwa Simba kumshawishi Nasreddine Nabi kujiunga na timu yao ikiwa itaachana na DimitarPantev, lakini Kocha huyo Mtunisia aliyewahi kuwanoa watani wao Yanga, anaonekana kuwa mtu sahihi wa kuiongoza timu yao.
Alichokifanya Nabi ndani ya ardhi ya Tanzania akiwa na kikosi cha Yanga, kimempa heshima kubwa na thamani kubwa na ikiwa Simba itaamua kumchukua, uamuzi huo unaonekana utakubaliwa na Wanasimba wengi.
Ameshinda mataji manne akiwa na Yanga, moja akiwa na FAR Rabat na moja akiwa na Kaizer Chiefs.
Nabi mwenye umri wa miaka 60, kwa sasa hana timu tangu alipoachana na Kaizer Chiefs, Oktoba mwaka huu.