Home Habari za michezo HERSI AFUNGUKA USAJILI MZITO WA OKELLO

HERSI AFUNGUKA USAJILI MZITO WA OKELLO

17
0

RAIS wa klabu ya Yanga, Hersi Said, ameweka wazi juu ya mchakato wa usajili wa nyota wa Uganda, Allan Okello, akibainisha kuwa klabu hiyo ipo katika hatua za kufuatilia kwa karibu uwezekano wa kumsajili ama katika dirisha dogo la usajili la mwezi Januari au dirisha kubwa la mwezi Juni.

Kauli ya Hersi imekuja wakati Okello akihusishwa vikali kufanya mazungumzo na mabingwa hao wa Tanzania kwa ajili ya kujiunga na kikosi hicho kinachoshiriki mashindano ya ndani na ya kimataifa, jambo lililoendelea kuzua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki wa Yanga.

Akizungumza kuhusu nyota huyo, Hersi amesema uongozi wa Yanga umekuwa ukimfatilia Okello kwa muda mrefu, hata kabla hajakwenda kucheza soka la kulipwa nchini Algeria, jambo linaloonesha kuwa usajili huo haukuwa wa ghafla.

Hersi ameeleza kuwa alivutiwa na uwezo wa Okello tangu mwaka 2019, alipofanya safari maalumu nchini Uganda kwa lengo la kuwafuatilia wachezaji kadhaa wenye vipaji, akiwemo Okello pamoja na Bobosi na Mustafa Kizza.

“Nakumbuka mwaka 2019 nilienda Uganda kumfuatilia yeye, Bobosi na Mustafa Kizza. Niliona uwezo wake na nikampenda Okello. Muda sio mrefu tutamsajili, kama sio Januari basi ni Juni,” amesema Hersi.

Kauli hiyo imeongeza matumaini kwa mashabiki wa Yanga ambao wanaendelea kusubiri kwa hamu kuona nyota huyo wa Uganda akivalia jezi ya kijani na njano, huku uongozi wa klabu ukisisitiza kuwa kila hatua ya usajili inazingatia maslahi ya timu kwa sasa na baadaye.