Home Habari za michezo DAVIES PHIRI ATAMBULISHWA MSIMBAZI

DAVIES PHIRI ATAMBULISHWA MSIMBAZI

55
0

UONGOZI  wa Klabu ya Simba umeendelea kuimarisha benchi la ufundi baada ya kumtambulisha rasmi Davies Phiri kama kocha mpya wa makipa wa kikosi hicho.

Phiri amesaini mkataba wa miaka miwili, hatua inayolenga kuongeza ubora na ushindani katika eneo la ulinzi wa lango la Simba.

Phiri, ambaye ana umri wa miaka 49, ni raia wa Zambia na amejiunga na Simba akitokea klabu ya Amazulu FC ya Afrika Kusini, ambako alikuwa akihudumu kama kocha wa makipa. Uzoefu wake katika soka la Afrika Kusini unatajwa kuwa faida kubwa kwa wekundu wa Msimbazi.

Kabla ya kuingia kwenye ukocha, Davies Phiri alikuwa kipa mahiri aliyewahi kuitumikia klabu ya Golden Arrows ya Afrika Kusini, sambamba na kuitumikia Timu ya Taifa ya Zambia maarufu kama Chipolopolo, akijijengea heshima kubwa katika soka la ukanda wa Kusini mwa Afrika.

Phiri ataungana na kocha mkuu Steve Barker kuunda benchi la ufundi imara litakalokuwa na jukumu la kuiongoza timu kwenye mashindano mbalimbali ya ndani na kimataifa kuanzia msimu huu na kuendelea.

Uongozi wa Simba unaamini kuwa ujio wa Phiri utaongeza ushindani miongoni mwa makipa wa kikosi hicho, sambamba na kuboresha viwango vyao vya kiufundi na kisaikolojia, jambo linalotarajiwa kuleta matokeo chanya ndani ya uwanja.

Tayari Phiri amewasili nchini na ameanza kazi rasmi ya kujiunga na kikosi hicho kinachoendelea na maandalizi ya michuano ya Mapinduzi Cup, huku mashabiki wa Simba wakitarajia kuona mabadiliko chanya katika safu ya ulinzi wa lango la timu yao.