Home Habari za michezo MFUNGAJI BORA MALAWI KUTUA MSIMBAZI

MFUNGAJI BORA MALAWI KUTUA MSIMBAZI

50
0

KLABU ya Simba imefikia hatua za mwisho za mazungumzo na mabingwa wa Malawi, Nyasa Big Bullets, kwa lengo la kunasa saini ya winga mahiri Chikumbutso Salim maarufu kama Chiku Salim katika dirisha dogo la usajili.

Taarifa za ndani zinaeleza kuwa pande zote mbili zimeridhiana kwa kiasi kikubwa, huku kilichobaki kikiwa ni kukamilisha taratibu chache kabla ya mchezaji huyo kutangazwa rasmi kuwa mali ya Wekundu wa Msimbazi.

Salim amekuwa kwenye kiwango bora msimu huu baada ya kuonyesha makali yake katika Ligi Kuu ya Malawi, akicheza jumla ya mechi 28 na kufanikiwa kufunga mabao 15 pamoja na kutoa asisti 11, rekodi inayomweka miongoni mwa wachezaji hatari zaidi kwenye ligi hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, nyota huyo alifanikiwa pia kuibuka kuwa mfungaji bora  wa Ligi ya Malawi hadi kufikia Desemba 27, jambo lililovutia macho ya klabu kadhaa barani Afrika, lakini Simba ikaonekana kuwa mbele zaidi katika mbio za kumsajili.

Ujio wa Salim unatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa Simba kuimarisha safu ya ushambuliaji, hasa eneo la winga, kuelekea nusu ya pili ya msimu na mashindano ya ndani pamoja na yale ya kimataifa.

Iwapo dili hilo litakamilika kama inavyotarajiwa, Salim ataungana na kikosi cha Simba akitarajiwa kuongeza ushindani, kasi na ubunifu katika safu ya mbele.