Home Habari za michezo NDANI YA MASAA 48 JANGWANI KUTAMBULISHA WAPYA

NDANI YA MASAA 48 JANGWANI KUTAMBULISHA WAPYA

53
0

UONGOZI wa Klabu ya Yanga umeweka wazi kuwa mchakato wa usajili bado unaendelea, leo na kesho wakitarajiwa kuendelea kuwatambulisha nyota wapya wa kimataifa watakaokiongeza nguvu kikosi hicho kuelekea michuano ijayo.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema klabu hiyo bado haijafunga rasmi dirisha la usajili na ndani ya siku mbili zijazo mashabiki watarajie taarifa nyingine njema kuhusu wachezaji wapya.

Kamwe ameeleza kuwa uongozi umejipanga kikamilifu kuhakikisha kikosi kinakuwa imara zaidi, hasa kwa kuongeza wachezaji wenye ubora na uzoefu wa kimataifa ili kukidhi malengo makubwa ya klabu ndani na nje ya nchi.

Hadi sasa, Yanga tayari imethibitisha usajili wa nyota watatu, ambapo wawili ni Mohammed Damaro na Marouf Tchakei waliotua kwa mkopo kutoka Singida Black Stars, huku usajili wa tatu ukiwa ni mzawa Emmanuel Mwanengo aliyechukuliwa kutoka TRA United.

Kwa mujibu wa Kamwe, usajili wa wachezaji wazawa tayari umefikia tamati, na sasa nguvu zote zinaelekezwa kwa nyota wa kigeni wanaotarajiwa kuongeza ushindani na ubora ndani ya kikosi cha Wananchi.

“Hatujamaliza usajili bado, tunatarajia kutangaza nyota wengine wawili kama siyo leo (Jumatatu) basi kesho (Jumanne). Kuhusu wazawa tayari tumeshafunga ukurasa,” amesema Kamwe,