SIMBA imefanikiwa kukata tiketi ya kucheza hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Fufuni SC katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar.
Kiungo wa Simba, Naby Camara, alikuwa shujaa wa mchezo huo baada ya kufunga bao la ushindi dakika ya 90, bao lililowahakikishia Wekundu wa Msimbazi nafasi ya kuendelea na safari yao katika michuano hiyo.
Hata hivyo, Simba ilianza mchezo huo kwa kushtukizwa baada ya Fufuni SC kupata bao la mapema dakika ya 15 lililofungwa na Mbonj Steven, jambo lililoifanya Simba kuongeza kasi ya mashambulizi wakisaka bao la kusawazisha.
Juhudi za Simba zililipa dakika ya 23 baada ya Hussein Mbegu kufunga bao la kusawazisha, bao lililorejesha matumaini kwa mashabiki wa timu hiyo na kuwafanya wachezaji kuendelea kushambulia kwa umakini mkubwa.
Mchezo uliendelea kuwa wa ushindani mkubwa hadi dakika za mwisho, ambapo Camara alitumia vyema nafasi aliyopata na kuifungia Simba bao la pili, lililohitimisha ushindi wa 2-1 na kuzima kabisa matumaini ya Fufuni SC.
Kwa matokeo hayo, Simba sasa inatinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi ambako itakutana na Azam FC, timu iliyofanikiwa kuiondoa URA ya Uganda kwa ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo mwingine wa robo fainali.