Home Habari za michezo SAKATA LA CONTE NA DOUMBIA KAMWE AFICHUA

SAKATA LA CONTE NA DOUMBIA KAMWE AFICHUA

26
0

OFISA Habari wa Klabu ya Yanga, Ali Kamwe, amefunguka kuhusu sakata linalowahusu nyota wao wawili, Balla Conte na Mohammed Doumbia, wanaodaiwa kugoma kutolewa kwa mkopo kwenda Singida Black Stars.

Yanga na Singida Black Stars zilikuwa zimefikia makubaliano ya kubadilishana wachezaji, ambapo Marouf Tchakei na Mohamed Damaro wamejiunga  na kikosi cha Wananchi, huku Conte na Doumbia wakielekea kujiunga na Walima Lizeti kwa mkopo.

Hata hivyo, mpango huo haujakamilika baada ya nyota hao kushindwa kujiunga na Singida Black Stars, huku zikiibuka taarifa kwamba wamegoma na kudai kulipwa fedha zao pamoja na kuvunja mikataba yao, jambo ambalo uongozi wa Yanga umelikataa.

Kutokana na msimamo huo, Yanga imeendelea kuwajumuisha Conte na Doumbia katika kikosi chake kilichopo visiwani Zanzibar kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi, hatua iliyolenga kuonyesha kuwa bado ni sehemu ya timu.

Akizungumza kuhusu suala hilo, Kamwe amesema wachezaji hao bado ni mali ya Yanga na wapo kambini Zanzibar pamoja na timu, huku akisisitiza kuwa taarifa nyingi zinazoandikwa hazina ukweli.

“Hao wachezaji ni mali ya Yanga na wapo na timu hapa Zanzibar. Kuna watu wamekuwa wanaandika vitu tofauti tofauti, lakini kama kutakuwa na suala lolote la kutolewa kwa mkopo au kusitisha mikataba yao, taarifa rasmi itawekwa wazi,” amesema Kamwe.